VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI VYAONGOZA UWASILISHAJI WA KAZI ZA SAMIA KALAMU AWARDS 2026

DAR ES SALAAM. 

Vyombo vya habari vya mtandaoni vinaongoza kwa kuwasilisha kazi za kuwania Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo za Samia Kalamu Awards (SKA) 2026, huku jumla ya kazi 624 zikiwa zimewasilishwa hadi Juni 15, 2026.

Taarifa iliyotolewa na waandaaji wa tuzo hizo, ambao ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) pamoja na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imeeleza kuwa kazi 276 sawa na asilimia 44 ya kazi zote zilizowasilishwa zimetoka katika vyombo vya habari vya mtandaoni.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, magazeti yamewasilisha kazi 178 sawa na asilimia 29, televisheni kazi 102 sawa na asilimia 16, redio kazi 60 sawa na asilimia 10 huku majarida yakichangia kazi nane pekee, sawa na asilimia moja ya kazi zote zilizopokelewa. 

Aidha, kati ya kazi zote zilizowasilishwa, kazi 20 sawa na asilimia 4.8 zimewasilishwa katika kundi la tuzo za vyombo vya habari, kazi 25 sawa na asilimia 4.0 katika kundi la tuzo maalum za kitaifa na kazi 569 sawa na asilimia 91.2 katika makundi ya tuzo za kisekta. 

Waandaaji wa tuzo hizo wameeleza kuwa mwitikio huo mkubwa unaonesha kuongezeka kwa matumizi ya majukwaa ya kidijitali katika uzalishaji na usambazaji wa habari za maendeleo, pamoja na dhamira ya waandishi wa habari nchini kuendelea kuelimisha, kuhabarisha na kuhamasisha jamii kuhusu maendeleo ya taifa. 

Wamewapongeza waandishi wa habari na vyombo vya habari ambavyo tayari vimewasilisha kazi zao, huku wakiwahimiza wale ambao bado hawajakamilisha mchakato huo kutumia muda uliosalia kuwasilisha kazi zao kabla ya kufungwa kwa dirisha la maombi.

Taarifa hiyo imekumbusha kuwa dirisha la kupokea kazi za kuwania Samia Kalamu Awards 2026 litafungwa rasmi Juni 30, 2026 saa 5:59 usiku, na kwamba kazi zinazostahili kushindanishwa ni zile zilizochapishwa au kurushwa kati ya Julai 1, 2025 na Juni 30, 2026. 

Samia Kalamu Awards ni jukwaa la kitaifa lililoanzishwa kwa lengo la kutambua, kuthamini na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari za maendeleo nchini kupitia kaulimbiu ya “Kalamu kwa Maendeleo.” 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.