WEST KILIFOREST TOUR CHALLENGE 2026 YAVUTIA WASHIRIKI ZAIDI YA 350

Zaidi ya washiriki 350 kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejitokeza kushiriki mashindano ya West Kili Forest Tour Challenge 2026 yaliyofanyika katika Shamba la Miti West Kilimanjaro, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, yakilenga kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, utalii wa misitu na afya kupitia michezo.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya kaulimbiu ya “Experience the Difference, Explore Life in Nature” yalihusisha mbio za kilomita 5, 10 na 21, mashindano ya baiskeli, pikipiki, matembezi ya misituni pamoja na shughuli mbalimbali za utalii wa mazingira.

Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo Leo Juni 21,2026, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, alisema tukio hilo limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Siha kama kitovu cha utalii wa asili na michezo huku likichochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi kupitia biashara mbalimbali zinazohusiana na utalii.

Dkt. Timbuka aliipongeza TFS kwa kuendelea kuandaa mashindano hayo na kusema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha yanaendelea kukua na kuvutia washiriki wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Hellen Mwambeta, alisema mashindano hayo yamechangia kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, kuimarisha afya na wakati huo huo kuongeza mzunguko wa fedha kupitia huduma zinazotolewa kwa wageni wanaofika kushiriki tukio hilo.

Mratibu wa mashindano hayo, Mensieur Elly, alisema washiriki wa mwaka huu walitoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania pamoja na Kenya na Uganda, huku wageni wengine wakitokea Ujerumani na Scotland, jambo linaloonesha kuongezeka kwa umaarufu wa mashindano hayo kimataifa.

Naye Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti West Kilimanjaro, PCO. Robert Faida, alisema West Kili Forest Tour Challenge ni sehemu ya juhudi za TFS za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kupitia michezo na utalii endelevu, huku ikitoa fursa kwa washiriki kujifunza kuhusu umuhimu wa kulinda mfumo wa ikolojia wa Kilimanjaro.

Mwisho wa mashindano hayo, washiriki wote walitunukiwa medali za kumbukumbu kwa kutambua mchango wao katika kuhamasisha michezo, utalii wa misitu na uhifadhi wa mazingira,na washindi mbalimbali walipewa zawadi huku TFS ikiahidi kuendelea kuimarisha tukio hilo ili liwe moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo na utalii nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.