CHAMA cha Mbio za Magari Tanzania (AAT), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, kimeendelea kutekeleza mradi wa FIA Safe and Sustainable Mobility Grant Programme unaolenga kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wenye umri chini ya miaka 18 katika shule 19 za msingi na sekondari zilizopo Wilaya ya Ubungo, ili kupunguza ajali zinazowakumba watoto.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo ya utekelezaji wa mradi huo wa elimu ya Usalama wa Barabarani Mashuleni ,Kamishna Msaidizi wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu, Joseph Mwakabonga, amesema watoto ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kupata ajali kutokana na ongezeko la vyombo vya usafiri na msongamano wa magari, hasa katika maeneo ya shule.
Aidha ameongeza kuwa ajali za barabarani zinaendelea kusababisha vifo, majeruhi na ulemavu wa kudumu, huku watembea kwa miguu, waendesha baiskeli, waendesha pikipiki na watoto wakiwa makundi yanayoathirika zaidi.
Mwakabonga amesisitiza kuwa suluhisho la changamoto hiyo ni kuanza kuwajengea watoto uelewa wa usalama barabarani tangu wakiwa shuleni ili wajifunze matumizi sahihi ya barabara na kuheshimu sheria za usalama.
"Usalama barabarani si jukumu la Jeshi la Polisi pekee, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuanzia Serikali, taasisi, shule, wazazi hadi wananchi kwa ujumla."
Pia amewataka madereva wa vyombo vyote vya usafiri kuzingatia sheria za usalama barabarani, akibainisha kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa jamii
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Utawala wa AAT, Hanif Virji, amesema kupitia mradi huo, AAT imetekeleza maboresho mbalimbali katika shule 19 za Wilaya ya Ubungo ikiwemo kutoa elimu kwa wanafunzi na walimu pamoja na kuboresha miundombinu ya usalama kwa kuweka alama za barabarani, michoro ya usalama, vivuko vya waenda kwa miguu (zebra crossing) na matuta ya kupunguza mwendo wa magari.
Amefafanua zaidi lengo la mradi huo ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama wanapoingia na kutoka shuleni, sambamba na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa usalama barabarani katika familia na jamii zao.


Hakuna maoni: