Tanzania imekubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Ufugaji wa Nyuki barani Afrika yatakayofanyika jijini Algiers, Algeria, tarehe 3-6 Septemba, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari wa televisheni za Algeria kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers, Balozi Mobhare Matinyi alisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, ndiye atakayefungua maonesho hayo kwa niaba ya serikali.
Balozi Matinyi alisema Mhe. Waziri Dkt. Kijaji atakuja Algeria akiongoza ujumbe wa maafisa waandamizi na wataalamu wa serikali pamoja na wadau kutoka sekta binafsi ya ufugaji wa nyuki na utengenezaji wa bidhaa za nyuki nchini.
Balozi Matinyi alisema serikali inaipa sekta ya ufugaji wa nyuki umuhimu wa kipekee kwani inaajiri watu wapatao milioni mbili nchini na huingiza dola za Marekani milioni 77.5 (shilingi bilioni 205) kwa mwaka kutokana na mauzo ya asali katika nchi mbalimbali duniani.
Akinukuu takwimu za serikali, Balozi Matinyi alisema Tanzania hivi sasa ni ya pili kwa uzalishaji asali barani Afrika na ya kumi duniani na bado ikijipanga zaidi ina uwezo wa kufikisha mizinga ya nyuki takribani milioni 9.2 yenye uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali na tani 9,200 za nta kwa mwaka.
Bw. Benchouia aliambatana na Mwenyekiti wa Baraza la Kisayansi la taasisi inayoandaa maonesho hayo, Dkt. Abdelmadjid Bouchareb, pamoja na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Biashara cha Dunia hapa Algeria, Bw. Ahmed Tibaoaoui.
Maonesho hayo maarufu kwa jina la Africa Bee Expo 2026, yanafanyika kwa mara ya nne hapa Algeria na Tanzania inatarajia kuonesha mafanikio yake katika sekta hii na kujifunza kutoka kwa wafugaji na wazalishaji wa bidhaa za nyuki wa nchi zingine.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania,
Algiers, Julai 20, 2026.


Hakuna maoni: