TANZANIA YAPENDEKEZA KUIMARISHWA USHIRIKIANO KATI YA MABUNGE YA NCHI WANACHAMA WA OACPS

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Sillo (Mb.), amewasilisha mapendekezo ya Tanzania yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na kuboresha upatikanaji wa taarifa kwa wabunge ili kuongeza ufanisi wa ushiriki wao katika shughuli za Jumuiya.

Mapendekezo hayo yametolewa wakati wa mazungumzo kati ya Mhe. Sillo na Katibu Mkuu wa OACPS, Mhe. Moussa Saleh Batraki, yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, Julai 21, 2026.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Sillo amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano wa Samoa kwa kuzingatia misingi ya usawa, ushirikishwaji na manufaa ya pamoja kwa nchi wanachama.

Aidha, Mhe. Sillo amesema Bunge litaendelea kushirikiana na OACPS kuimarisha ushirikiano na kuunga mkono utekelezaji wa mageuzi yatakayoiwezesha Jumuiya kuhudumia nchi wanachama kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa OACPS, Mhe. Batraki, amesema Sekretarieti ya OACPS inaendelea kutekeleza maboresho yatakayowezesha programu zake kuendana na mahitaji na vipaumbele vya nchi wanachama, yakilenga kuimarisha ushirikiano kati ya mabunge pamoja na kujenga mifumo endelevu ya kifedha kwa ajili ya shughuli za Jumuiya.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Nyamanga, amesema Tanzania inaendelea kuunga mkono utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano wa Samoa na ajenda nyingine za maendeleo ili kuhakikisha nchi wanachama zinanufaika kikamilifu na fursa za zinazotolewa na jumuiya.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.