Dar es Salaam, Julai 4, 2026
ACT-Wazalendo imeitaka Serikali kumaliza mara moja tatizo la mgao wa maji unaoendelea kuathiri maeneo mbalimbali nchini, ikisema mamilioni ya wananchi hawawezi kuendelea kubeba gharama za uzembe, ubadhirifu na usimamizi dhaifu wa sekta ya maji.
Akizungumza kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri Kivuli wa Maji wa ACT Wazalendo, Yasinta Cornely Awiti, alisema wananchi wa maeneo yanayohudumiwa na DAWASA, ikiwemo Ubungo, Kimara, Mbezi, Tabata, Kurasini, Tegeta, Bunju, Kigamboni na maeneo mengine, pamoja na baadhi ya mikoa, wameendelea kukabiliwa na upatikanaji duni wa maji, huku wengine wakipata huduma hiyo mara moja kwa wiki au kutopata kabisa.
Chama hicho kilidai matatizo hayo yanasababishwa na uzembe katika usimamizi wa miradi, ubadhirifu wa fedha za umma na kushindwa kuwawajibisha wahusika. Pia kilieleza wasiwasi wake kuhusu kile kilichodai kuwa ni mipango ya kubinafsisha miundombinu ya maji kupitia ubia.
ACT Wazalendo pia ilinukuu ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zikionyesha changamoto za sekta hiyo, ikitolea mfano Mradi wa Maji wa Same–Mwanga–Korogwe unaodaiwa kupoteza takribani asilimia 70 ya maji yanayozalishwa.
Chama hicho kimeiomba Serikali kukomesha mgao wa maji, kukamilisha na kukagua miradi yote ya maji, kuwachukulia hatua waliohusika na ubadhirifu, kuwawajibisha viongozi wa mamlaka za maji walioshindwa kutekeleza majukumu yao, kusitisha mipango ya kubinafsisha sekta hiyo na kuelekeza fedha za Mfuko wa Maji katika kuboresha miundombinu ya huduma za maji.



Hakuna maoni: