Dar es Salaam.
Chama cha ACT Wazalendo kimetaka kufanyika kwa uchunguzi huru na wa haraka kuhusu uchaguzi wa viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kikieleza kuwa mchakato huo umeibua maswali makubwa kuhusu uhalali, uwazi na uaminifu wake.
Kupitia taarifa iliyotolewa Julai 10, 2026 na Waziri kivuli wa Maliasili, Utalii, Utamaduni na Michezo wa chama hicho, Emmanuel Ntobi, ACT Wazalendo imesema imefuatilia kwa karibu uchaguzi huo na kubaini madai yanayohitaji uchunguzi wa kina.
Kwa mujibu wa chama hicho, taarifa walizozipata kutoka kwa baadhi ya wajumbe, wapigakura na wadau zinaonyesha kuwa katika uchaguzi wa nafasi ya Rais wa TOC, Anthony Mtaka alipata kura 29, Henry Tandau kura sita na Leonard Thadeo kura moja kati ya kura 36 zilizopigwa, lakini baadaye Thadeo akatangazwa mshindi wa uchaguzi huo.
ACT Wazalendo pia imeeleza kuwa sintofahamu hiyo imekuja baada ya mchakato wa uchaguzi wa TOC kuahirishwa mara kadhaa tangu mwaka 2024, huku baadhi ya wagombea wakienguliwa na baadaye kurejeshwa kufuatia maelekezo ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC). Aidha, chama hicho kimekumbusha kuwa Aprili 10, 2026, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paulo Makonda, alisimamisha uchaguzi uliokuwa ufanyike Aprili 12, akavunja uongozi uliokuwepo na kuteua uongozi wa mpito.
Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimetoa wito kwa IOC, Chama cha Kamati za Olimpiki Afrika (ANOCA) pamoja na mamlaka husika nchini kuanzisha uchunguzi wa mchakato mzima wa uchaguzi ili kubaini ukweli wa matokeo yaliyotangazwa na kuchukua hatua stahiki endapo kutabainika ukiukwaji wa sheria au kanuni. Pia kimesema tayari kimewasilisha barua rasmi kwa IOC kuomba uchunguzi huo ufanyike.
ACT Wazalendo imesisitiza kuwa wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za AFCON 2027, ni muhimu kulinda hadhi ya nchi kwa kuhakikisha taasisi za michezo zinaendeshwa kwa misingi ya haki, uwazi, demokrasia na utawala bora.

Hakuna maoni: