SERIKALI YAONGEZA NGUVU MATENGENEZO YA BARABARA KUPITIA MPANGO WA CBRM

Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam.

Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imezindua Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara unaoshirikisha Jamii (Community-Based Routine Maintenance - CBRM), utakaotekelezwa kwa miaka mitatu kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya barabara, kutoa ajira na kuongeza ushiriki wa wananchi katika utunzaji wa barabara.

Akizungumza Katika Maonyesho ya 50 ya kimataifa ya biashara Sabasaba kuhusu utekelezaji wa mpango huo, Mratibu wa CBRM kutoka TARURA Makao Makuu, Mhandisi Richard Missa, alisema mpango huo unatekelezwa chini ya Mradi wa RISE unaosimamiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI na TARURA kwa ufadhili wa mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 hadi 2027/2028, mpango huo unatarajiwa kutunza zaidi ya kilomita 15,000 za barabara nchini, isipokuwa Mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na kunufaisha zaidi ya vikundi 3,000 vya wananchi kupitia ajira na fursa za kujiongezea kipato.

Mhandisi Misa alisema lengo jingine la mpango huo ni kujenga utamaduni wa wananchi kumiliki na kulinda miundombinu ya barabara kwa kuwashirikisha moja kwa moja katika shughuli za matengenezo ya kawaida.

Alifafanua kuwa vikundi vitakuwa vikifanya kazi za kufyeka nyasi kandokando ya barabara, kuzibua mifereji, makaravati na madaraja, kuondoa vikwazo vinavyozuia matumizi ya barabara pamoja na kusafisha na kukarabati alama za barabarani ili kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote wa mwaka.

Aidha, alisema utekelezaji wa mwaka wa kwanza tayari umeanza katika mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro na Dodoma, ambapo zaidi ya kilomita 1,500 za barabara zimefanyiwa matengenezo kupitia vikundi 302 vya jamii.

Kwa mujibu wa Mhandisi Misa, vikundi vinavyoshiriki vinapaswa kuwa vinatoka katika maeneo yaliyo karibu na barabara husika, visivyozidi umbali wa kilomita tano, huku kila kikundi kikipewa mkataba wa kazi wenye siku 100 ili kuwawezesha wananchi kupata kipato sambamba na kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi.

Aliongeza kuwa mbali na kazi za matengenezo ya barabara, wanufaika watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali yatakayowawezesha kuwa na shughuli endelevu hata baada ya kukamilika kwa mikataba yao.

Mhandisi Misa alibainisha kuwa mpango wa CBRM pia unatekeleza maelekezo ya Serikali yanayotaka asilimia 30 ya bajeti ya matengenezo ya barabara kuelekezwa kwenye vikundi vya jamii vinavyotumia nguvu kazi, huku akisisitiza kuwa mpango huo hauondoi nafasi ya makandarasi wa kawaida bali unakamilisha jitihada za kuhakikisha barabara zinakuwa salama na zinapitika katika misimu yote ya mwaka.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.