DCEA YAELIMISHA WANAHABARI KUHUSU KEMIKALI BASHIRIFU NA MBINU MPYA ZA BIASHARA HARAMU YA DAWA ZA KULEVYA
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini DCEA imeendesha semina maalum kwa wanahabari ili kuwajengea uwezo wa kutambua na kuripoti kwa usahihi masuala yanayohusu kemikali bashirifu na dawa mpya za kulevya zinazotumika na wahalifu.
Akizungumza katika semina hiyo, Florence Kambi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa DCEA, amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na wahalifu kubuni mbinu mpya kila siku.
Amesema baadhi ya mbinu hizo ni pamoja na kubadilisha maumbo ya bidhaa mbalimbali, kutumia bidhaa za kawaida kama vifungashio vya dawa za kulevya, pamoja na kutumia kemikali tofauti zinazoweza kuficha au kubadilisha asili ya dawa hizo.
“Wauzaji, wazalishaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya wamekuwa wabunifu zaidi, hivyo tunalazimika sisi pia kuboresha elimu na mbinu za ufuatiliaji,” amesema Kambi.
Changamoto ya teknolojia na taarifa potofu
Bi Kambi ameeleza kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili bandia (AI), yameongeza changamoto katika upatikanaji wa taarifa sahihi, hasa pale ambapo data zisizo sahihi zinaweza kusambaa mtandaoni.
Amesema ni muhimu taasisi husika kuhakikisha zinaweka taarifa sahihi mtandaoni ili wananchi na wanahabari waweze kupata uelewa wa kweli kuhusu dawa za kulevya na kemikali hatarishi.
Wito kwa wanahabari
Wanahabari wametakiwa kuwa sehemu muhimu ya mapambano hayo kwa kuhakikisha wanaripoti taarifa zilizo sahihi na zilizoidhinishwa na mamlaka husika, ili kusaidia jamii kuepuka madhara ya dawa za kulevya.
DCEA imeendelea kusisitiza kaulimbiu yake ya uelimishaji: “Kataa dawa za kulevya, timiza malengo yako.”
Semina hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za serikali kuongeza uelewa kwa umma kuhusu hatari za dawa za kulevya na kemikali bashirifu, ambazo zimekuwa zikitumika kwa njia mpya katika biashara haramu duniani.





Hakuna maoni: