Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameshiriki katika Mkutano Mkuu wa Afrika ulioandaliwa na African Leadership Magazine kwa kushirikiana na African Leadership Organization (ALO), unaofanyika jijini London, Uingereza.
Mkutano huo umewakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, taasisi za maendeleo, wasomi na wadau mbalimbali kutoka Afrika na maeneo mengine duniani kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Bara la Afrika, yakiwemo uongozi, uwekezaji, biashara na ushindani wa kiuchumi. Mkutano huo umeongozwa na kaulimbiu isemayo: “From Vision to Velocity: Driving Africa’s Next Wave of Growth & Leadership.”
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Washauri ya African Leadership Organization (ALO), aliongoza kikao cha Bodi hiyo kilichojadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Afrika pamoja na mikakati ya kuimarisha uongozi bora, uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu ya bara hilo.
Bodi ya Washauri ya ALO inaundwa na viongozi na wataalamu mashuhuri kutoka nchi mbalimbali duniani. Miongoni mwa wajumbe wake ni Jewel Howard Taylor, Makamu wa Rais Mstaafu wa Liberia; Tahir Akhtar, Mkurugenzi wa Adam Global Holdings (Uingereza/Umoja wa Falme za Kiarabu); Victor Oladokun wa African Development Bank; Christian Lindfeld, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Africa Ventures Advisory nchini Ujerumani; William E. Ward, Kamanda Mkuu Mstaafu wa Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika; Nomvula Mokonyane, Naibu Katibu Mkuu wa African National Congress (ANC); pamoja na Ken Giami, Mtendaji Mkuu wa African Leadership Organization (ALO).
Ushiriki wa Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Kikwete katika mkutano huo unaendelea kudhihirisha nafasi yake katika majukwaa ya kimataifa yanayojadili mustakabali wa Afrika, hususan katika kuhamasisha uongozi wenye maono, ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na maendeleo jumuishi na endelevu ya Bara la Afrika.



Hakuna maoni: