DAR ES SALAAM.
Bodi ya Bima ya Amana imewahakikishia wananchi kuwa fedha wanazoweka katika benki na taasisi za fedha zilizosajiliwa zinalindwa kisheria, huku ikiwataka kutembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) – Sabasaba ili kupata elimu kuhusu huduma zake na umuhimu wa bima ya amana.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la bodi hiyo, Afisa wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Joyce Shala, alisema bodi hiyo ni taasisi ya serikali iliyoanzishwa kwa lengo la kulinda amana za wateja, kulipa fidia kwa wanaostahili endapo benki au taasisi ya fedha itafilisika, pamoja na kudumisha imani na utulivu wa mfumo wa kifedha nchini.
Alisema bodi hiyo hukusanya michango kutoka benki na taasisi za fedha, huwekeza fedha za mfuko ili kuimarisha uwezo wa kulipa fidia kwa wakati, na pia husimamia mchakato wa ufilisi wa benki kwa lengo la kupunguza hasara kwa wateja na kulinda mfumo wa fedha kwa ujumla.
Shala alibainisha kuwa katika utekelezaji wa majukumu hayo, asilimia 99 ya wateja waliostahili walirejeshewa asilimia 100 ya fedha zao, huku kesi zilizobaki zikiwa chini ya mazingira maalumu ya kisheria.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali kutembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) ili kupata elimu ya bure kuhusu bima ya amana, huduma zinazotolewa na haki za waweka amana.





Hakuna maoni: