VETA WABUNI MTAMBO MAALUMU WA KUVUNA SENENE RAFIKI WA MAZINGIRA

DAR ES SALAAM. 

Wakati juhudi za kulinda mazingira zikiendelea kupewa kipaumbele nchini, ubunifu wa teknolojia za ndani unaendelea kuwa suluhisho muhimu la kupunguza athari zinazotokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Miongoni mwa ubunifu huo ni mtambo maalumu wa kisasa wa kuvuna senene uliobuniwa na Chuo cha Ufundi Stadi cha Kagela (Kagela VTC), ukiwa na lengo la kuboresha uvunaji huku ukihifadhi mazingira.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mwalimu wa Kagela VTC, Elias Lucas Mayala, amesema mtambo huo, ambao pia unatumika kama mtego wa kisasa wa kuvuna senene, umetengenezwa ili kupunguza uharibifu wa miti na kulinda mazalia ya senene unaosababishwa na mbinu za jadi zinazotumiwa na baadhi ya wavunaji.

Mayala amesema mtambo huo unagharimu takribani Sh700,000 na una uwezo wa kubeba kati ya kilo 80 hadi 100 za senene kwa wakati mmoja wa uvunaji. Ameongeza kuwa umewekewa mfumo maalumu wa kuchuja senene na kuwatenganisha wadudu wadogo, ambao badala ya kupotea wanaweza kutumika kama chakula cha kuku na hivyo kuongeza thamani ya mabaki yanayopatikana wakati wa uvunaji.

Ameeleza kuwa mtambo huo umetengenezwa kwa mfumo unaorahisisha matumizi yake, ikiwemo uwezo wa kusogezwa kwa urahisi kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na mahitaji ya wavunaji. Amesisitiza kuwa matumizi ya mtambo huo yanasaidia kuongeza ufanisi wa uvunaji huku yakipunguza athari kwa mazingira ikilinganishwa na mbinu za kawaida.

Aidha, amewahimiza wananchi wanaojihusisha na uvunaji wa senene kuachana na mbinu zinazoharibu mazingira na badala yake kutumia mtambo huo wa kisasa ili kulinda mazingira na kuongeza tija katika shughuli zao.

Pia amewaalika wadau, wajasiriamali na wananchi wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kufika katika banda la VETA kwa ajili ya kujionea ubunifu huo, kupata elimu zaidi pamoja na kununua au kutengenezewa mtambo huo kulingana na mahitaji yao.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.