Meneja wa Miradi ya Nishati wa Umoja wa Ulaya (European Union – EU), Massimiliano Pedretti, amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo ni msingi muhimu wa kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya nishati nchini.
Akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) lililofanyika wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Pedretti amesema miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme inahitaji uwekezaji mkubwa wa kifedha ambao hauwezi kutegemea Serikali pekee, hivyo ni muhimu wadau wote kushirikiana katika kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha.
Amesema Umoja wa Ulaya unaendelea kuunga mkono maendeleo ya sekta ya nishati nchini kupitia utoaji wa ruzuku za mitaji (capital grants) kwa miradi midogo ya nishati pamoja na kusaidia kutafuta na kuwezesha masuluhisho ya kifedha kwa miradi mikubwa ya kimkakati inayohitaji uwekezaji mkubwa.
Pedretti ametoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa hizo kwa kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya miradi (proposals) yenye ubora na yenye lengo la kutatua changamoto za nishati nchini, ili yaweze kufanyiwa tathmini na kuangaliwa namna bora ya kuyawezesha kupata ufadhili.
Aidha, amesema Serikali ina jukumu la kuendelea kuweka sera na mazingira wezeshi yanayovutia uwekezaji, huku taasisi za fedha zikihimizwa kubuni bidhaa na huduma za kifedha zitakazorahisisha upatikanaji wa mitaji kwa wawekezaji wa sekta ya nishati.
Ameeleza kuwa taasisi za kimataifa za fedha na washirika wa maendeleo zipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kufadhili miradi ya nishati, lakini mafanikio yake yanategemea uwepo wa miradi iliyoandaliwa kwa viwango vinavyokubalika kimataifa, mifumo madhubuti ya usimamizi pamoja na mazingira yanayojenga imani kwa wawekezaji.
Kwa mujibu wa Pedretti, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo kutachochea uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati, kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa.

Hakuna maoni: