GAVANA DKT. TUTUBA: SABASABA NI JUKWAA LA KUCHOCHEA UCHUMI,BOT YAENDELEA KUJENGA MFUMO SALAMA WA MATUMIZI YA SARAFU ZA KIDIJITALI
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameendelea kujidhihirisha kuwa kitovu cha biashara, uwekezaji na utoaji wa elimu kwa umma, huku yakitoa fursa kwa taasisi za umma na sekta binafsi kusogeza huduma karibu na wananchi na kuimarisha maendeleo ya uchumi wa taifa.
Akizungumza baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho ya 50 ya Sabasaba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dkt. Emmanuel Tutuba, alisema mafanikio ya maonesho hayo yanaonesha ukuaji wake mkubwa, huku ushiriki wa mataifa zaidi ya 25 ukithibitisha hadhi yake ya kimataifa.
Maonesho hayo yanawapa Watanzania nafasi ya kupata huduma, elimu ya kifedha, kujifunza teknolojia mpya pamoja na kufahamu fursa mbalimbali zinazochochea biashara na uwekezaji.
Akizungumzia sera ya fedha, Tutuba alisema uamuzi wa BOT kuweka kiwango cha riba cha asilimia 6.25 umefanywa kwa kuzingatia hali ya uchumi na lengo la kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei pamoja na kuimarisha utulivu wa mfumo wa fedha.
Kiwango hicho kitasaidia kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, kuongeza ukwasi katika mabenki ya biashara ili yaendelee kutoa mikopo kwa sekta mbalimbali za uzalishaji na kudumisha utulivu wa bei za bidhaa na huduma.
Aidha, amesema kuingia kwa msimu wa mavuno kunatarajiwa kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania kutokana na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni, hali itakayowanufaisha wakulima na wafanyabiashara wanaouza bidhaa katika masoko ya nje.
Kuhusu matumizi ya sarafu za kidijitali na mali za mtandaoni (virtual assets), Tutuba alisema Benki Kuu ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi ya sheria na kanuni zitakazosimamia sekta hiyo.
"Tumeshaandaa concept note pamoja na rasimu ya sheria na kanuni. Sasa tunazipeleka kwenye vyombo vingine ikiwemo Wizara ya Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Baraza la Mawaziri na hatimaye Bungeni," alisema.
Amefafanua kuwa mfumo huo wa kisheria unalenga kuweka mazingira salama ya matumizi ya sarafu za kidijitali kwa kudhibiti vihatarishi kama utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na kulinda uwekezaji wa Watanzania.
Kwa upande wa elimu ya fedha, Tutuba alisema BOT imeendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia banda lake pamoja na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania.
Amesema mwitikio umekuwa mkubwa na kwamba tayari zaidi ya watu 200 wamejiandikisha kushiriki programu maalumu ya mafunzo ya elimu ya fedha itakayofanyika mwezi Novemba.
Gavana Dkt. Tutuba amewahakikishia Watanzania kuwa sekta ya benki nchini inaendelea kuwa imara, ikiwa na mitaji ya kutosha, faida endelevu na uwezo wa kutoa huduma kwa ufanisi, huku soko la dhamana za Serikali likiendelea kuimarika na kuchangia uthabiti wa mfumo wa fedha nchini.









Hakuna maoni: