Dar es Salaam.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kuimarisha usimamizi wa ubora wa miradi ya ujenzi wa miundombinu nchini kupitia maabara zake za kisasa zinazofanya uchunguzi na uhakiki wa vifaa vya ujenzi pamoja na kazi zinazotekelezwa hatua inayochangia kujenga miundombinu imara, salama na yenye kudumu kwa muda mrefu.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Fundi Sanifu kutoka Kitengo cha Utafiti na Udhibiti Ubora TARURA Makao Makuu, Jacob Manguye amesema maabara hizo zina jukumu muhimu la kuhakikisha miradi yote ya barabara, madaraja na miundombinu mingine inazingatia viwango vya kitaalamu na masharti ya mikataba kabla na baada ya utekelezaji.
Amesema wataalamu wa maabara hufanya vipimo vya kina vya vifaa vya ujenzi kabla havijatumika kwenye miradi sambamba na kuhakiki ubora wa kazi zinazotekelezwa na wakandarasi ili kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
"Tunafanya uhakiki wa kazi mbalimbali ikiwemo za vifusi, lami, madaraja na miundombinu mingine ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na ubora wa hali ya juu na inadumu kwa muda mrefu", amesema Manguye.
Amebainisha kuwa kwa sasa TARURA ina maabara kuu iliyopo Makao Makuu Dodoma pamoja na maabara nyingine 14 zilizosambazwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Kigoma, Arusha na Moshi. Maabara hizo zinatoa huduma za upimaji wa vifaa vya ujenzi na uhakiki wa ubora wa miradi kwa lengo la kuongeza ufanisi na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mbali na hilo, amesema TARURA inamiliki mtambo maalumu wa uchunguzi wa udongo (Geotech) unaowezesha kufanya tafiti za kina kuhusu uwezo wa udongo kuhimili ujenzi wa madaraja, majengo na miundombinu mingine mikubwa kabla ya ujenzi kuanza hatua inayosaidia kupunguza hatari za uharibifu wa miundombinu na kuongeza usalama wa watumiaji.
Manguye ametoa wito kwa wakandarasi, wahandisi, taasisi za ujenzi na wadau wengine wa sekta hiyo kutumia huduma za maabara za TARURA ili kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inafikia viwango vinavyotakiwa na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.


Hakuna maoni: