Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amepongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha ulinzi, usalama na amani nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Julai 6, 2026, Dkt. Nyansaho amesema juhudi za vyombo hivyo zimeendelea kuhakikisha nchi inabaki kuwa salama, hali inayowapa wananchi fursa ya kufanya shughuli za kiuchumi na maendeleo bila hofu.
Amesema amani na utulivu vinavyoendelea kushuhudiwa nchini ni msingi muhimu wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na mipango mingine ya maendeleo.
Dkt. Nyansaho amesema JKT, mbali na jukumu lake la msingi la kulinda na kujenga uzalendo, linaendelea kutekeleza shughuli za uzalishaji mali pamoja na kutoa mafunzo kwa vijana yanayowawezesha kujitegemea na kujiajiri.
Aidha, amesema ushiriki wa JKT na JWTZ katika maonesho hayo umetoa fursa kwa wananchi kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hizo, ikiwemo huduma zinazotolewa kwa jamii, uzalishaji mali na programu za mafunzo kwa vijana.
Katika hatua nyingine, amesema kampuni ya usafi na unyunyuzi wa dawa ya SUMAJKT imeendelea kutoa ajira kwa vijana, ambapo hadi sasa imefanikiwa kuajiri vijana 4,800, jambo linaloonesha mchango wa JKT katika kupunguza changamoto ya ajira nchini.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuziimarisha taasisi hizo ili ziendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Hakuna maoni: