Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) imesema ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) unalenga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, kuwaelimisha kuhusu matibabu ya kibobezi na kuonesha teknolojia za kisasa zinazotumika kuokoa maisha ya wagonjwa.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema taasisi hiyo imejikita katika nguzo tatu kuu ambazo ni utoaji wa huduma za kibobezi, mafunzo kwa wataalamu wa afya na utafiti unaolenga kuboresha huduma za matibabu kulingana na mazingira na vinasaba vya Waafrika.
Amesema MOI imeanzisha mifumo ya kidijitali inayowawezesha wananchi kujisajili na kuweka miadi ya kumuona daktari wakiwa majumbani mwao kupitia simu za mkononi au kwa kuscan QR Code, hatua inayopunguza msongamano hospitalini na kuokoa muda wa wagonjwa.
"Mwananchi hatalazimika tena kufika hospitalini alfajiri kusubiri huduma. Anaweza kupanga miadi mapema akiwa popote na kufika kwa wakati aliopangiwa," amesema.
Amesema katika banda la MOI lililopo Sabasaba, wananchi wanapata huduma za uchunguzi na ushauri kutoka kwa madaktari bingwa wa mifupa na mishipa ya fahamu, huku wakielimishwa kuhusu magonjwa mbalimbali yanayohusu ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu.
Aidha, amesema taasisi hiyo imeonesha maendeleo makubwa katika utengenezaji wa viungo bandia kwa kutumia teknolojia ya 3D Printing, inayowezesha kutengeneza vifaa vinavyoendana na maumbo ya miili ya wagonjwa, ikiwemo mikono ya kisasa inayotumia betri yenye uwezo wa kushika na kuachia vitu.
Balozi Dkt. Ulisubisya amesema MOI pia inaendelea kutumia mtambo wa kisasa wa Cathlab (Angio Suite) kutibu magonjwa mbalimbali ya mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua kichwa, kuziba au kufungua mishipa iliyopata hitilafu, kutibu matatizo ya uti wa mgongo pamoja na kusaidia wagonjwa wenye maumivu sugu kwa kuelekeza dawa katika eneo husika kwa usahihi mkubwa.
Amesema licha ya kutoweza kuhamisha vifaa vikubwa kama CT Scan, MRI na X-ray katika maonesho hayo, taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kuhusu huduma hizo na mafanikio yake katika kuokoa maisha ya wagonjwa.
Katika maonesho hayo pia, baadhi ya wagonjwa waliopata matibabu MOI wametoa ushuhuda wa mafanikio yao, akiwemo mgonjwa aliyekuwa ameshindwa kutembea kwa zaidi ya miaka minane lakini sasa ameweza kurejea katika maisha yake ya kawaida baada ya kufanyiwa matibabu ya kibobezi.
Akizungumzia maadhimisho ya taasisi hiyo, Balozi Dkt. Ulisubisya amesema mwaka huu ni wa kipekee kwa kuwa wakati Maonesho ya Sabasaba yanaendelea kuelekea kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, MOI nayo inaadhimisha miaka 30 ya utoaji wa huduma za kibingwa na kibobezi.
Amesema katika kipindi hicho cha miaka 30, MOI imefanikiwa kupanua huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, kuwekeza katika teknolojia za kisasa za matibabu, kuimarisha mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya tafiti zinazochangia kuboresha huduma za matibabu, hatua ambazo zimechangia kupunguza rufaa za wagonjwa waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
Aidha, amesema taasisi hiyo kitafanya mazungumzo na TANTRADE ili kuwa na kituo cha kudumu katika eneo la Sabasaba kitakachotoa huduma za awali za afya, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakazi wa Mbagala, Mtoni, Azizi Ali na maeneo jirani, huku wagonjwa wanaohitaji huduma za kibobezi zaidi wakiendelea kupatiwa rufaa kwenda MOI.


Hakuna maoni: