Lindi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary, amesema Mkoa wa Lindi umeanza kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia lengo la kitaifa la kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Bi. Omary amesema hayo leo, Julai 15, 2026, alipokutana na Afisa Mshauri Mwandamizi wa Masuala ya Kiufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Deusdedit Malulu, aliyeambatana na uongozi wa Kampuni ya Tango Energy Limited, inayotekeleza usambazaji wa majiko banifu mkoani Lindi.
“Nawapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Tunamuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na tutaendelea kutoa elimu ili iwafikie wananchi wote,” amesema Bi. Omary.
Kwa upande wake, Mha. Malulu amesema jumla ya majiko banifu 5,776 yameanza kusambazwa na Kampuni ya Tango Energy Limited katika maeneo ya Lindi, Ruangwa, Nachingwea, Liwale na Kilwa.
Mha. Malulu amewataka wananchi katika maeneo hayo kuchangamkia fursa ya kupata majiko banifu kwa bei nafuu ya ruzuku ya shilingi 7,600 tu kwa jiko.
Naye, Meneja wa Mauzo wa Tango Energy Limited, Bw. Emmanuel Ibrahim, amesema mradi huo unahusisha usambazaji wa majiko banifu yanayotumia kiasi kidogo cha kuni na mkaa, hatua inayolenga kupunguza matumizi ya vyanzo hivyo vya nishati pamoja na athari za moshi unaotokana na matumizi ya majiko ya kawaida.
Kupitia mradi huo, Tango Energy Limited itasambaza jumla ya majiko banifu 5,776 kwa wananchi kwa bei ya ruzuku. Bei halisi ya jiko moja ni TZS 50,847.46, lakini Serikali imetoa ruzuku ya asilimia 85, hivyo mwananchi atanunua jiko kwa TZS 7,600 tu.





Hakuna maoni: