RAIS SAMIA KUTUNUKU WASHINDI WA VIJANA UCHUMI CHALLENGE KESHO JNICC

RAIS SAMIA KUTOA TUZO ZA VIJANA UCHUMI CHALLENGE JNICC JULAI 5, 2026

Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa washindi wa shindano la kitaifa la Vijana Uchumi Challenge 2026, itakayofanyika Julai 5, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo mshindi wa kwanza ataondoka na Sh milioni 100.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ofisi ya Rais anayeshughulikia maendeleo ya vijana Joel Arthur Nanauka, amesema shindano hilo limeanzishwa kwa lengo la kuwapa vijana jukwaa la kutumia ubunifu, maarifa na vipaji vyao kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia ujasiriamali, teknolojia na suluhisho za changamoto za kijamii na kiuchumi.

Amesema serikali imekusudia kuibua, kutambua na kuendeleza mawazo bunifu ya vijana kwa kuyaunganisha na taasisi za kifedha, wataalamu, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo ili yaweze kutekelezwa na kuleta manufaa kwa jamii.

Kuhusu zawadi, Waziri Nanauka amesema mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh milioni 100, mshindi wa pili Sh milioni 50 na mshindi wa tatu Sh milioni 20, huku washindi wengine saba wakipatiwa zawadi mbalimbali kwa kutambua ubunifu wao.

Ameongeza kuwa mpango huo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwajengea mazingira ya kubadili mawazo yao kuwa miradi yenye tija, ajira na mchango katika maendeleo ya Taifa.

Serikali imewahimiza vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini kuendelea kubuni miradi yenye tija na kutumia fursa zinazotolewa kupitia programu hiyo ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.