SAMIA ATOA TSH TRILIONI 6.23 KUKAMILISHA SGR TABORA–KIGOMA, BABA LEVO ASEMA NI MWANZO WA FURSA
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu Baba Levo, amesema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kutoa Shilingi trilioni 6.23 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma, utakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 14, 2026, katika Kituo Kikuu cha Reli ya Kisasa (SGR) jijini Dar es Salaam, Baba Levo alisema mradi huo utabadilisha sura ya usafiri na biashara kwa kuunganisha Kigoma moja kwa moja na Dar es Salaam kupitia reli ya kisasa ya mwendo wa kasi.
Alisema ujenzi wa reli hiyo unatarajiwa kufungua maelfu ya fursa za ajira, huku akieleza kuwa zaidi ya ajira 15,000 zinatarajiwa kupatikana kupitia utekelezaji wa mradi huo.
"Mradi huu ni mkombozi kwa wananchi wa Kigoma na maeneo ya jirani. Utafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na ajira. Wananchi wanapaswa kujiandaa kuutumia kujijengea uchumi," alisema Baba Levo.
Aliongeza kuwa uzinduzi wa mradi huo unatarajiwa kufanyika Julai 20, 2026 na kuongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku ukitarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi pamoja na wasanii mbalimbali aliowataja kuwa ni "watoto wa Mama", akiwemo Diamond Platnumz, Alikiba, Chino Kidd na wengine.
Baba Levo pia alisema stesheni ya SGR itakayojengwa Kigoma itakuwa ya nne kwa ukubwa nchini, jambo alilosema linaonesha dhamira ya Serikali ya kuifanya Kigoma kuwa kitovu muhimu cha uchumi na usafirishaji katika ukanda wa Magharibi.
"Stesheni itakayojengwa Kigoma itakuwa ya nne kwa ukubwa nchini. Nimshukuru sana Rais Samia na uongozi wa TRC kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika mkoa wetu," alisema.
Aidha, alisema Rais Samia anatarajiwa pia kuzindua meli iliyokuwa imesimama kwa muda mrefu, hatua ambayo itaimarisha usafiri na biashara katika Ziwa Tanganyika.
Kwa upande wake, Baba Levo alisema ameamua kugharamia behewa zima la treni litakalowabeba wananchi bure kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma ili kushiriki uzinduzi wa mradi huo.
Akihitimisha, aliwataka wananchi wa Kigoma kuupokea mradi huo kwa matumaini makubwa, akisisitiza kuwa reli ya kisasa itafungua ukurasa mpya wa maendeleo.
"Mmezoea kusema Kigoma ni mwisho wa reli. Kuanzia sasa isiitwe tena mwisho wa reli, bali mwanzo wa fursa," alisema.

Hakuna maoni: