Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametembelea banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amejionea mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya umeme na teknolojia mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Julai 13, 2026, Mhe. Dkt. Mwinyi alipata fursa ya kujionea miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme, teknolojia za matumizi bora ya umeme ikiwemo majiko sanifu yanayotumia umeme kwa ufanisi, huduma ya Luku Janja pamoja na mfumo wa Smart House unaomwezesha mtumiaji kufuatilia matumizi ya umeme kupitia simu ya mkononi.
Akitoa maelezo kwa Mhe. Rais, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kujenga njia mpya tatu za kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar kupitia nyaya zitakazopita chini ya bahari.
Ameeleza kuwa njia hizo zitajumuisha Dar es Salaam–Unguja, Tanga–Pemba na Kisiju–Mafia, na kwamba kukamilika kwake kutaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na uwezo wa kuhudumia ongezeko la mahitaji ya umeme yanayotokana na ukuaji wa viwanda, sekta ya utalii, uwekezaji na shughuli nyingine za kiuchumi visiwani Zanzibar.
Bw. Twange amesema Serikali pia inaendelea kutekeleza mradi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 282, ambapo Dola milioni 6 zimetengwa mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea katika sekta ya umeme. Kupitia mradi huu wa Dola za Marekani milioni 282, tunaendelea kuimarisha miundombinu ya umeme, huku sehemu ya fedha hizo ikielekezwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme kwa kushirikiana na ZECO,” amesema Bw. Twange.
Aidha, amesema TANESCO imeendelea kuleta ubunifu wa kidijitali kupitia mfumo wa Smart House, unaomwezesha mwananchi kufuatilia matumizi ya umeme wa nyumba yake kupitia simu ya mkononi, hatua inayosaidia matumizi bora na yenye tija ya umeme.
Vilevile, Bw. Twange amesema mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme umefikia mafanikio makubwa, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wananchi waliopata majiko hayo wanaendelea kuyalipia kwa utaratibu wa makato kupitia ununuzi wa umeme wa LUKU, hatua inayorahisisha wananchi kumudu gharama za kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Jitihada hizo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme ya uhakika na kutumia nishati safi katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, ikiwemo katika Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, umeendelea kuweka msingi wa upatikanaji wa umeme wa kutosha unaowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.





Hakuna maoni: