Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imesema hatua ya kuingia katika mfumo wa Maktaba Mtandao wa Taifa itasaidia kusogeza huduma za maktaba kwa wananchi wengi zaidi ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo wakati wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba),na Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji Huduma za Maktaba wa TLSB, Dkt. Rehema C. Ndumbaro,
Amesema mfumo huo umeanzishwa kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa vitabu na taarifa kwa njia ya kidijitali.
Dkt Ndumbaro, amesema maendeleo ya teknolojia yamebadilisha namna watu wanavyotafuta maarifa, jambo ambalo limeifanya TLSB kuendelea kuboresha huduma zake ili ziendane na mahitaji ya sasa ya jamii.
Hata hivyo,Dkt. Ndumbaro,amesisitiza kuwa mfumo huo utawaruhusu wanafunzi, watafiti na wananchi wengine kupata rasilimali mbalimbali za kielimu bila kulazimika kufika katika majengo ya maktaba.
Amesemj huduma hizo zinatarajiwa kuongeza usomaji, kusaidia shughuli za utafiti na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa makundi tofauti ya wananchi.
Sanjari na hayo,Dkt. Ndumbaro amesema kuwa maonesho ya Sabasaba yamekuwa fursa muhimu kwa taasisi hiyo kukutana na wananchi, kuwaelimisha kuhusu huduma zinazopatikana na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Amesema TLSB inaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha huduma za maktaba nchini kwa kutumia teknolojia ili kuhakikisha maarifa yanawafikia wananchi wengi zaidi kwa urahisi.
Wananchi waliotembelea banda la TLSB katika maonesho hayo walipata fursa ya kujifunza kuhusu huduma za maktaba mtandao na namna ya kuzitumia katika shughuli zao za kila siku za kujifunza na kufanya utafiti.

Hakuna maoni: