TBA YANYAKUA TUZO YA PILI KATIKA BANDA BORA SABASABA 2026
Dar es Salaam.
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umefanikiwa kushika nafasi ya pili katika kipengele cha Banda Bora kwa upande wa Sekta ya Miliki na Real Estate kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yaliyohitimishwa Julai 13, 2026, jijini Dar es Salaam.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Bi. Amina Lumuli, kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Arch. Daud W. Kondoro. Amesema mafanikio hayo yametokana na maandalizi ya kitaalamu ya banda la TBA pamoja na namna lilivyowezesha wananchi na wadau kupata taarifa kuhusu huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Bi. Lumuli alisema TBA ilitumia maonesho hayo kuhamasisha uwekezaji kupitia miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), huku pia ikitoa elimu kuhusu miradi mikubwa ya ujenzi na maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Alieleza kuwa banda la TBA lilivutia idadi kubwa ya wageni waliotaka kujifunza kuhusu miradi ya nyumba za gharama nafuu, ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na kazi za ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya michezo, ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Sherehe za kufunga Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam na kukabidhi tuzo mbalimbali ziliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Katika maonesho hayo, TBA imeendelea kujidhihirisha kama miongoni mwa taasisi za umma zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma, ubunifu wa miradi na kuvutia uwekezaji nchini.


Hakuna maoni: