Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi ametembelea Banda la Kilimo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Akiwa kwenye maonesho hayo alitembelea Banda la Wadau wa Kilimo Ikolojia (TOAM)ambapo alielezewa namna ambavyo wadau hao wanavyofanya kazi.
Katika hotuba yake alisema, “Sekta ya Kilimo ni sekta ambayo ina mchango mkubwa sana kwenye suala zima la biashara kwa maana ya mazao yatokanayo na kilimo ni nguzo kubwa ya uingizwaji wa fedha iwe za kigeni na kwa zile zinazozunguka ndani ya nchi, naipongeza sekta hii kwa kazi nzuri ya kuwafikia na kuwawezesha wakulima.”
Akiwa kwenye Banda la Wadau wa Kilimo Ikolojia,(TOAM) Bw.Mbwasi amejionea namna ambavyo mbolea ya asili inavyofanya kazi na kuwahakikishia wadau hao kuwa Wizara itaendelea kufanya kazi nao pamoja katika kuyafikia masoko.
Kwa upande wake Afisa Ushawishi na Utetezi wa TOAM, Paul Chilewa amemwelezea Bw. Mbwasi kuwa TOAM inaendelea na utaratibu wa kuwawezesha wakulima kupitia vikundi na mkulima mmoja mmoja namna ya kutekeleza dhana ya KilimoBiashara katika Kilimo Ikolojia na mwitikio ni mzuri.




Hakuna maoni: