STEVE NYERERE KUFANYA IBADA MAALUMU YA KUWAENZI WANAHABARI, WASANII NA WADAU WA MICHEZO WALIOFARIKI DUNIA

Dar es Salaam. 

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama ongea na mwanao Steve Nyerere, amewaalika Watanzania kushiriki ibada maalumu ya kuwaombea na kuwaenzi wanatasnia wa habari, sanaa na michezo waliotangulia mbele ya haki, itakayofanyika kesho, Agosti 1, 2026, katika Viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Steve amesema ibada hiyo itawakutanisha wasanii, waandishi wa habari, wanamichezo, viongozi wa dini, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwaombea na kuwakumbuka watu walioacha alama kubwa katika tasnia hizo kabla ya kufariki dunia.

Amesema ibada hiyo si ya kundi maalumu pekee, bali ni ya kila Mtanzania aliyewahi kuguswa na kazi za wasanii, waandishi wa habari au wadau wa michezo waliotangulia mbele ya haki, akisisitiza kuwa ni wakati wa kuonyesha upendo, shukrani na kuthamini mchango wao kwa taifa.

"Endapo uliwahi kuguswa na kazi za msanii, mwandishi wa habari au mwanamichezo ambaye sasa ametangulia mbele ya haki, basi nakukaribisha ufike Leaders Club tushirikiane katika dua na sala za kuwaombea na kuwaenzi," amesema Steve.

Ameeleza kuwa miongoni mwa majina yatakayokumbukwa katika ibada hiyo ni pamoja na Steven Kanumba, King Majuto, Sharomilionea, Mzee Pwagu, Bini Hambilili, Hashimu Kambi, Stev2K na wengine wengi waliowahi kutoa mchango mkubwa katika tasnia za sanaa, habari na michezo.

Steve amesema lengo la ibada hiyo ni kuenzi maisha na mchango wa marehemu hao pamoja na kuendelea kudumisha utamaduni wa kukumbuka mema waliyoiachia jamii, akibainisha kuwa uwepo wa Watanzania wengi utakuwa ishara ya kuthamini kazi zao na urithi waliouacha.

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Leaders Club kesho, Agosti 1, 2026, ili kushiriki ibada hiyo ya pamoja ya dua na sala, akisisitiza kuwa kuwaenzi waliotangulia mbele ya haki ni sehemu ya kuenzi historia ya tasnia za habari, sanaa na michezo nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.