Makongamano na majukwaa yanayojadili mwenendo, changamoto na maendeleo ya sekta ya madini ni nguzo muhimu katika kuimarisha sekta hiyo na kuhakikisha inatoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Moses Kongola, kwa niaba ya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati akifunga kongamano la siku mbili lililoandaliwa na HakiRasilimali, lililojadili tafiti mbalimbali, maendeleo na nafasi ya Tanzania katika sekta ya madini mkakati.
Mhandisi Kongola amesema majukwaa hayo ni muhimu kwa kuwa yanatoa fursa kwa Serikali, wadau wa sekta ya madini, watafiti, wachimbaji na jamii kujadili kwa pamoja namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo na kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na utajiri wa madini nchini.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika uongezaji thamani madini nchini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi, hatua ambayo itasaidia kuongeza mapato ya Serikali, ajira na fursa za kiuchumi kwa Watanzania.
“Ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki katika kusimamia maendeleo ya sekta ya madini na kuhakikisha haki za jamii na wadau mbalimbali, wakiwemo wachimbaji wadogo, zinalindwa,” amesema.
Ameeleza kuwa Tanzania ina maeneo mengi yenye shughuli za uchimbaji madini, hivyo maafisa madini wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha haki za wachimbaji wadogo zinalindwa, huku Taratibu na Sheria za madini zikizingatiwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki zao, hususan kuhusu haki ya ardhi na haki ya madini, ili kuimarisha uelewa na kupunguza migogoro kati ya wamiliki wa leseni, wamiliki wa maeneo ya ardhi na wachimbaji.
Kuhusu mifumo ya kisera, Mhandisi Kongola amesema Wizara ya Madini imeandaa orodha ya madini mkakati yatakayotambuliwa rasmi na kuwekwa katika mfumo maalumu wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali hizo.
Kongamano hilo limelenga kujadili namna Tanzania inavyoweza kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa madini mkakati, huku majadiliano yakijikita katika uongezaji thamani wa madini, haki za jamii, elimu kwa umma, mifumo ya kisera, utafiti na uwajibikaji.
Mhandisi Kongola amesema Serikali itazingatia mawazo na mapendekezo yaliyotolewa na washiriki katika kongamano hilo, akisisitiza kuwa majadiliano ya aina hiyo ni muhimu katika kujenga sekta ya madini yenye tija, uwazi na manufaa kwa Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa HakiRasilimali, Dkt. Donald Kasongi, amempongeza mgeni rasmi kwa kukubali kushiriki na kufunga kongamano hilo, huku akiiomba Serikali kuyafanyia kazi maazimio na mapendekezo yaliyofikiwa na washiriki.
Dkt. Kasongi amesema utekelezaji wa maazimio hayo utasaidia kuhakikisha majadiliano yaliyofanyika yanazaa matokeo chanya na kuchangia katika maendeleo endelevu ya sekta ya madini nchini.









Hakuna maoni: