TARI YAHAMASISHA KILIMO CHA MBEGU BORA ZA MATUNDA NA VIUNGO NCHINI

WAKULIMA WASHAURIWA KUPANDA MITI YA MATUNDA NA VIUNGO VILIVYOFANYIWA UTAFITI KWA TIJA KIUCHUMI NA AFYA

Wakulima na wananchi kwa ujumla wameshauriwa kuwekeza katika upandaji wa miti ya matunda, migomba na viungo vilivyofanyiwa utafiti, kwa kuwa vina faida kubwa kiafya na kiuchumi.

Ushauri huo umetolewa na Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) – Tengeru, Emmanuel Pallangyo, wakati akizungumza na mwandishi wa Raia Mwema Digital katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba.

Amesema TARI inaendelea kufanya utafiti wa mazao mbalimbali yakiwemo miti ya matunda, viungo, mahindi, mpunga na mengine, ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora zinazozalisha kwa tija zaidi.

Pallangyo amesisitiza kuwa mazao kama ndizi, matunda na viungo vinaweza kulimwa hata kwenye bustani za nyumbani, hivyo kupunguza gharama za maisha na kuongeza kipato cha kaya.

“Hapa Sabasaba tunazo mbegu za mchaichai, parachichi, pera, migomba, korosho na nyingine nyingi. Tunawahamasisha wananchi waje wachukue mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na taasisi yao,” amesema.

Ameongeza kuwa mbegu zinazozalishwa na TARI zinazingatia tafiti za kisayansi ili ziweze kuendana na mazingira ya maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

“Tunahamasisha matumizi ya viungo kwenye vyakula na hata chai kwa sababu vinaboresha afya na kuongeza ladha ya chakula,” ameongeza.

Hata hivyo, Pallangyo amesema changamoto kubwa ni baadhi ya wakulima kuendelea kutumia mbegu za zamani ambazo hazina tija, hali inayochangia uzalishaji mdogo.

Kwa upande wake, mkulima wa migomba kutoka Chalenzi, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Martin Mayengela, amesema amevutiwa na mbegu za TARI na ameamua kununua miche ya migomba na parachichi kwa ajili ya kuipanda shambani kwake.

“Nimekuja hapa kununua miche ya migomba na parachichi ili niipande shambani kwangu. Naamini itanisaidia kupata matokeo mazuri,” amesema. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.