Mwanza.
Mpango wa Matengenezo ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (Community Based Routine Maintenance – CBRM) unaotekelezwa na Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) utasaidia kuondoa hoja mbalimbali na kuimarisha upatikanaji wa vikundi vya kijamii katika matengenezo ya kawaida ya barabara nchini.
Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira na Jamii, Dkt. Haledeus Makene wakati akifungua mafunzo ya mpango huo kwa Menejimenti, Mameneja wa Mikoa na Maofisa Ununuzi wa TARURA kutoka mikoa mbalimbali yanayofanyika jijini Mwanza.
Dkt. Makene amesema kuwa uundwaji wa vikundi hivyo utaleta mafanikio makubwa kwa Wakala huo na Serikali kwa ujumla kutokana na wanufaika wake kuwa wakazi wa maeneo husika hali inayowawezesha kumiliki na kulinda miundombinu inayowazunguka.
Amesema hatua hiyo itachangia barabara nyingi zinazosimamiwa na TARURA kupitika misimu yote kwani wananchi wenyewe watawajibika kuzitunza.
"Tunahitaji wananchi wenyewe wamiliki barabara zilizopo katika maeneo yao. Vikundi vinavyoundwa vitatoka katika maeneo yao na kufanya matengenezo ya kawaida mara kwa mara, hivyo kuwa walinzi wa miundombinu pia kuongeza kipato na kuinua hali zao kiuchumi", amesema Dkt. Makene.
Kwa upande wake, Mratibu wa CBRM, Mhandisi Richard Missa amesema mpango huo wa miaka mitatu unatarajiwa kutekelezwa katika halmashauri 70 zilizopo kwenye mikoa 25 ukiwa na lengo la kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara zenye urefu wa takribani kilomita 15,000.
Hata hivyo, Mhandisi Missa amesema tangu kuanza kwa mpango huo kilomita 7,000 tayari zimefikiwa.
Amesema moja ya majukumu ya TARURA ni kuhakikisha barabara zinapitika mwaka mzima hivyo vikundi hivyo vinapaswa kufanya kazi za kufyeka nyasi, kusafisha na kufungua mitaro ya maji pamoja na matundu ya makalavati ili hata wakati wa mvua miundombinu iwe salama na isilete uharibifu.
Naye, Mratibu wa Kitaifa wa Programu kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. Dampu Ndenzako ameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kushirikiana katika kujenga uwezo wa utekelezaji wa mpango huo hatua inayolenga kuleta mageuzi katika upitikanaji wa barabara mwaka mzima pamoja na kuwaongezea kipato wana kikundi.







Hakuna maoni: