Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimehimizwa kuwa na umoja wenye malengo katika kukabiliana na changamoto zinazoibuka duniani ambazo zisiposhughulikiwa ipasavyo zitakuwa na madhara makubwa katika usalama na uchumi wa nchi wanachama.
Hayo yamejiri Julai 16, 2026 mjini Salima, Malawi wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 28 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. James Millya akiambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud.
Tanzania katika Mkutano huo ambao jukumu lake kubwa ni kuratibu masuala ya amani na usalama katika nchi za SADC, imesisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati madhubuti wenye uwezo wa kubaini kwa haraka viashiria vya uvunjivu wa amani na vihatarishi vya uchumi katika Kanda hiyo.
Aidha, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. George Chaponda alieleza kuwa licha ya nchi za SADC kupiga hatua kubwa katika kuhamasisha mtangamano wa kikanda na utawala bora, bado majadiliano endelevu yanahitajika ili kuenzi mafanikio hayo kwa manufaa ya watu wa SADC.
Aliwataka Waheshimiwa Mawaziri kujadili agenda za mkutano huo kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa ambazo ni pamoja na kuheshimiana, uhuru, usawa, maridhiano, mshikamano na dhamira ya pamoja ili kuendeleza amani, usalama, demokrasia na maendeleo endelevu kwenye kanda.
Mkutano huo ulioanza na ngazi ya Makatibu Wakuu Julai 13, 2026 unajadili agenda mbalimbali zinazolenga kuhamasisha amani na usalama, demokrasia, utawala bora, maendeleo endelevu kwa kuhakikisha kuwa Kanda ya SADC inabaki tulivu wakati wote.




Hakuna maoni: