WIZARA YA NISHATI YAWAHAMASISHA WATOTO KUWA MABALOZI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Watoto wameaswa kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kulinda mazingira, kupunguza athari za kiafya zitokanazo na matumizi ya nishati zisizo safi na kufanikisha lengo la Taifa la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Wito huo umetolewa na Mhandisi Benezeth Kabunduguru kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, wakati akitoa elimu kuhusu nishati safi ya kupikia katika programu ya Play with Purpose Kids Tournament 2026 iliyoandaliwa na Potential Pioneers Initiatives na kufanyika katika Viwanja vya Pentagon, Ihumwa, mkoani Dodoma.

Akizungumza katika programu hiyo, Mhandisi Kabunduguru amesema watoto wana nafasi muhimu ya kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa kuelimisha familia zao na jamii kuhusu umuhimu wa kuachana na matumizi ya kuni, mkaa na mafuta ya taa na kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Akifafanua kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhandisi Kabunduguru amesema ni nishati isiyozalisha moshi wala uchafu unaoweza kuhatarisha afya wakati wa kupikia.

Ametaja aina za nishati hizo kuwa ni gesi ya kupikia (LPG), umeme, gesi asilia, biogas, bioethanol, mkaa mbadala na nishati ya jua.

Katika tukio hilo, Wizara ya Nishati ilikabidhi madaftari 250 kwa wanafunzi walioshiriki programu hiyo kwa lengo la kuimarisha uelewa wao kuhusu nishati safi ya kupikia na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii.

 Madaftari hayo yameandaliwa kwa mfumo wa maswali na majibu kuhusu maana ya nishati safi ya kupikia, sifa zake, aina zake na faida zake ili kuwasaidia watoto kujifunza kwa urahisi na kuendelea kueneza elimu hiyo shuleni, nyumbani na katika jamii kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.