Dodoma
Kampuni ya CDICD Group Limited imeendelea kuimarisha mnyororo wa thamani katika Sekta ya Madini kwa kuchakata madini ya black granite na kuzalisha bidhaa mbalimbali za ujenzi zinazouzwa katika soko la ndani na nje ya nchi, hatua inayochochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kukuza mauzo ya bidhaa zenye thamani.
Akizungumza jijini Dodoma kwenye Maonesho ya Nane Nane, Meneja wa CDICD, Shija Shimba, amesema kampuni hiyo imewekeza katika kiwanda cha kisasa cha uchakataji wa black granite kinachobadilisha mawe ghafi kuwa bidhaa mbalimbali zikiwemo countertops za majiko, paving stones, slabs za ujenzi na headstones zinazotumika katika makaburi.
Amesema shughuli za uchimbaji na uchakataji zinafanyika katika kijiji cha Manyemba, wilayani Chamwino mkoani Dodoma, ambapo kampuni imejikita katika kuongeza thamani ya madini kabla ya kuyapeleka sokoni.
Kwa mujibu wa Shimba, uwekezaji huo umeiwezesha CDICD kupanua masoko yake ndani na nje ya Tanzania. Mbali na kuuza bidhaa zilizochakatwa nchini, kampuni pia husafirisha black granite blocks kwenda China na nchi nyingine kwa ajili ya uchakataji zaidi katika viwanda vya nchi hizo.
Amesema kampuni huzalisha wastani wa tani 270 za black granite kwa wiki, huku bidhaa zake zikisambazwa kupitia vituo vya mauzo vilivyopo Dodoma na Victoria, Kinondoni jijini Dar es Salaam, pamoja na mikoa mbalimbali nchini.
Shimba amesema uwekezaji huo pia umefungua fursa za ajira kwa vijana kati ya 90 na 100 wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo uendeshaji wa mitambo, udereva, uchomeleaji na shughuli nyingine za uzalishaji.
Ameongeza kuwa CDICD ilianza shughuli zake mwaka 2014 na imeendelea kupanua shughuli za uchimbaji wa black granite katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chamwino, kabla ya kuhamishia shughuli zake Manyemba, ambako inaendelea na uzalishaji na uchakataji wa madini hayo kwa sasa.





Hakuna maoni: