IFCU YAWAINUA WAKULIMA IRINGA, WALIPWA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 5.5 KWA UFUTA


WAKULIMA wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Iringa (IFCU), katika mwaka wa fedha 2025/2026 wamelipwa zaidi ya shilingi bilioni 5.5 baada ya kuuza tani 237,000 za zao la ufuta.

Hayo yamesemwa Meneja wa IFCU, Tumaini Lupora wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Viwanja wa Nzuguni mkoani Dodoma, ambapo maonesho ya Nanenane yanafanyika Kitaifa.

Amesema chama chao kimekuwa mkombozi wa wakulima mkoani hapo hasa kwa kuhakikisha wanapata pembejeo za kilimo kwa wakati, hali ambayo inawawezesha kufuata misimu ya kilimo.

"Kupitia ushirika wa IFCU msimu wa 2022/2023 tulikusanya kilo 800,607 za ufuta ambapo wakulima walilipwa zaidi ya Shilingi bilioni 1.69. Na katika mwaka wa fedha 2025/2026 tumekusanya zaidi ya tani 237,800 na wakulima wamelipwa zaidi ya Shilingi bilioni 5.553," amesema.

Ameongeza kuwa IFCU ina vyama vya ushirika 63 katika Wilaya za Mufindi, Kilolo na Iringa, na vinahudumia wakulima wanachama 862 pamoja na wakulima wengine zaidi ya 50,000 wasio wanachama.

Lupora amesema chama hicho kimeshiriki kwa mara ya tatu mfululizo katika Maadhimisho ya Nanenane kitaifa yanayofanyika Jijini Dodoma, kwa kuonesha bidhaa mbalimbali zenye thamani ya lishe zinazozalishwa na wakulima wa mkoa huo.

"Tumekuja na bidhaa kama maharage lishe. Haya ni maharage yenye virutubisho vya ziada ikiwemo madini ya chuma na zinki pamoja na protini. Madini haya ni muhimu sana katika ujenzi wa afya ya binadamu na kusaidia kupunguza utapiamlo kwa watoto," amesema.

Meneja huyo amesema mbali na maharage lishe, IFCU imeonesha pia unga wa mahindi ya njano ambapo utafiti umeonyesha mahindi haya yana Vitamin A zaidi ukilinganisha na mahindi ya kawaida. Mtu anapoyala anapata virutubisho vya ziada," ameongeza. 

Amesema pia katika mabanda yao wana bidhaa kama karanga, mahindi na ufuta, jambo ambalo linamhakikishia mkulima maisha bora.

Lupora amesema kupitia mfumo wa ushirika, wakulima wa Iringa wameondokana na tatizo la kuuza nazao yao kwa vipimo visivyo rasmi kama "madebe" na "magunia" ambavyo vilikuwa vikiwadhulumu.

Meneja huyo amesema IFCU inatarajia katika mpango wake wa miaka 5 kuanzia 2026 hadi 2030 kuwafikia wakulima 100,000 na kuwapa elimu ya kilimo bora ya kilimo hai ili kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Mkulima na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Mufindi, Paul Mwinuka amesema amepata elimu na kunufaika na pembejeo za ruzuku zinazoletwa hadi kijijini.

"Nilikuwa nalima ekari 10 tu, baada ya kujiunga na ushirika sasa nalima zaidi ekari 50 na kila ekari navuna zaidi ya gunia 20 za mahindi. Mwaka jana bei za mahindi ziliporomoka, IFCU ilituunganisha na NFRA na tukapata soko. Hivi sasa wameingia mkataba wa kununua tani 5,000 za mahindi," amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la We Effect Tanzania, Frank Ademba amesema shirika hilo linafanya kazi na IFCU kupitia programu ya "Kuboresha Maisha na Haki ya Chakula". 

"Lengo ni kuwajengea uwezo taasisi, kukuza kilimo ikolojia na kilimo endelevu, kuzingatia jinsia na mabadiliko ya tabianchi. Tumemsaidia IFCU kulima mazao yenye lishe kwa sababu Iringa inaongoza kwa utapiamlo," amesema Ademba.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.