JUKWAA la Wanawake Vijijini Tanzania (RWA Tanzania) limeainisha maeneo ya kipaumbele yanayolenga kuimarisha sauti, uongozi na ushiriki wa wanawake wa vijijini katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
Hayo yamesemwa na Mwanajukwaa wa RWA Tanzania, Judith Singibala, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane Nzuguni, mkoani Dodoma.
Singibala amesema jukwaa hilo, lililoanzishwa mwaka 2023, ni mtandao wa wanawake wa vijijini ambao umeendelea kukua kwa kasi, ukiwa na wanachama 2,473 kutoka mikoa mbalimbali nchini. Amesema lengo lake ni kuimarisha sauti, uongozi na ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
"Jukwaa linawaunganisha wanawake wadogo wakulima, wafugaji, wavuvi, wahifadhi wa mbegu za asili na wengine wanaotegemea rasilimali za asili kwa maisha yao. Matokeo yamekuwa mazuri kwa wanachama wetu," amesema.
Ametaja mojawapo ya maeneo yanayotekelezwa na RWA Tanzania kuwa ni kuhamasisha kilimo cha kiikolojia kwa kutoa elimu kuhusu matumizi ya mbinu za kilimo zisizotegemea kemikali zinazoweza kuharibu udongo na mazingira.
Aidha, amesema jukwaa hilo linafundisha utengenezaji wa mbolea za asili na viuatilifu vya kibaolojia ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima wadogo, sambamba na kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kupitia uhifadhi wa udongo na uvunaji wa maji.
Singibala amesema wanawake hao pia wanaanzisha na kusimamia benki za mbegu katika ngazi ya jamii kwa lengo la kulinda na kuhifadhi mbegu za asili zinazotishiwa kutoweka.
"Vilevile tunaendesha mfumo wa ubadilishanaji wa mbegu kati ya wakulima wa ndani na wanajukwaa wa kikanda, kupitia ushirikiano wetu na wanawake kutoka Madagascar, Zambia, Lesotho na Zimbabwe," amesema.
Ameongeza kuwa RWA Tanzania inatetea uhuru wa mbegu ili kupunguza utegemezi wa mbegu za viwandani na kurejesha umiliki wa mbegu mikononi mwa wakulima.
Kwa upande wa haki za wanawake, amesema jukwaa hilo linaelimisha jamii kuhusu haki za wanawake kurithi, kumiliki na kutumia ardhi kwa ajili ya uzalishaji. Pia linajenga uwezo wa wanawake kushiriki kikamilifu katika vyombo vya maamuzi kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, huku likipinga mfumo-dume na ukatili wa kiuchumi unaokwaza maendeleo ya wanawake.
Singibala amesema eneo jingine la kipaumbele ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuhamasisha wanawake wa vijijini kushiriki katika kampeni endelevu za upandaji miti kwa ajili ya kulinda mazingira na kujenga mustakabali wa kijani.
Aidha, amesema jukwaa hilo linashughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, ikiwemo kupambana na imani potofu, ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa rasilimali na tofauti za kiuchumi zinazowaathiri wanawake wa vijijini.
Amesema RWA Tanzania ni sehemu ya mtandao wa Rural Women's Assembly unaofanya kazi katika nchi mbalimbali barani Afrika kwa lengo la kujenga mshikamano wa wanawake wa vijijini na kutetea haki zao.









Hakuna maoni: