Asema watumiaji wamefikia asilimia 28.6 mwaka 2025 kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021
Na Mwandishi Wetu - KIZIMKAZI, ZANZIBAR
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.), amesema idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia imeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 28.6 mwaka 2025, hatua anayoeleza kuwa ni matokeo ya juhudi zinazoendelea za Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo nchini.
Mhe. Ndejembi ameyasema hayo leo, Agosti 11, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika Mdahalo wa Nishati Safi unaofanyika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, ukiwakutanisha viongozi na wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kujadili namna ya kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema ongezeko hilo limechangiwa na hatua mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034.
“Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ilizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024/2034. Tangu kuzinduliwa kwa mkakati huo, tumeshuhudia kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kupitia kampeni na maonesho ya nishati safi, kuanzishwa kwa miradi ya utoaji wa ruzuku katika mitungi ya majiko na kaya zilizoko vijijini, pamoja na uanzishwaji wa miradi ya utoaji majiko ya umeme kupitia bili ya umeme (on-bill finance),” amesema Mhe. Ndejembi.
Waziri Ndejembi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa wananchi, sambamba na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuhatarisha afya.
“Tuliwakopesha wateja na habari njema ni kuwa utaratibu ule ulifanikiwa kwa zaidi ya asilimia 95. Sisi tumetengeneza ubia na wasambazaji binafsi ambapo tunakwenda sasa kukopesha majiko milioni moja,” amesema Bw. Twange.
Amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za TANESCO kuongeza matumizi ya umeme kama nishati safi ya kupikia na kuwawezesha wananchi kupata majiko ya umeme kwa utaratibu unaorahisisha uwezo wao wa kumudu gharama.
Akizungumzia upatikanaji wa umeme Zanzibar, Bw. Twange amesema TANESCO kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), wanatarajia kutekeleza mradi wa kuongeza kiwango cha umeme kinachosafirishwa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar, hatua itakayosaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme katika visiwa hivyo.
“Tuna mradi wa kuongeza kiwango cha umeme unaotoka Tanzania Bara kuja huku. Tumepata mdau wa maendeleo, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), dola za Marekani milioni 282, zaidi ya shilingi bilioni 600 za Tanzania. Tunakwenda kutengeneza njia tatu za kupita chini ya maji, moja kuja Unguja, nyingine kwenda Pemba na nyingine kwenda Mafia,” amesema.
Mdahalo huo umeandaliwa na Mwanamke Initiative Foundation, chini ya Mkurugenzi wake Mhe. Wanu Hafidh Ameir, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, na umeambatana na maonesho ya wadau wa nishati safi ya kupikia yanayofanyika katika Hoteli ya Kwanza, Kizimkazi.





Hakuna maoni: