KAMPUNI ya Organic Moringa Limited imeitoa rai kwa jamii kutumia bidhaa zinazotokana na mlonge, ikieleza kuwa zina virutubisho vinavyoweza kuchangia katika lishe.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Sebastian Msapalla, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni jijini Dodoma.
Msapalla amesema kampuni hiyo imeendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali za asili kwa kutumia mimea yenye virutubisho, ikiwemo mlonge, uwi, rosela, mbegu za chia, mchele wa kahawia pamoja na asali inayozalishwa katika mazingira yenye miti ya mlonge.
Amesema lengo la kampuni hiyo ni kuwapatia wananchi bidhaa zinazotokana na maliasili na zinazoweza kutumika kama sehemu ya lishe yenye virutubisho.
Miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo ni unga wa majani ya mlonge, ambao hutengenezwa kwa kuzingatia taratibu za usindikaji kwa lengo la kuhifadhi virutubisho vinavyopatikana kwenye majani hayo.
Msapalla amesema bidhaa hiyo imeandaliwa kwa matumizi ya binadamu na inaweza kutumika kuongeza virutubisho katika lishe.
Aidha, Organic Moringa imekuja na bidhaa nyingine inayojulikana kama Moringa Root Powder, ambayo ni unga unaotokana na mzizi wa mlonge.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, bidhaa hiyo hutumika katika tiba asili, huku ikisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.


Hakuna maoni: