Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa kutatokea baridi kali nchini kutokana na tukio la Aphelion, ikisema taarifa hiyo si ya kweli.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA Agosti 9, 2026, taarifa hiyo ilidai kuwa kuanzia saa 11:00 alfajiri kwa muda wa saa 27, Tanzania ingeshuhudia tukio la Aphelion litakaloambatana na baridi kali kuliko kawaida, hali ambayo ingeweza kusababisha mafua, kikohozi na matatizo ya kupumua.
TMA imesema Aphelion ni tukio la kawaida katika mzunguko wa Dunia kwenye mfumo wa Jua, ambapo Dunia hufikia hatua ya kuwa mbali zaidi na Jua. Hata hivyo, imeeleza kuwa mchango wa tukio hilo katika mwenendo wa hali ya baridi kati ya msimu mmoja na mwingine ni mdogo sana katika maeneo ya Tanzania kutokana na nchi kuwa karibu na Ikweta.
TMA imeongeza kuwa kwa kawaida, kipindi cha Juni hadi Agosti ni majira ya Kipupwe katika maeneo mengi nchini, ambapo mifumo ya hali ya hewa hutawaliwa na baridi pamoja na upepo mkali. Utabiri wa msimu wa Kipupwe uliotolewa Mei 25, 2026 ulionyesha kuwa maeneo mbalimbali nchini yalitarajiwa kuwa na viwango tofauti vya baridi na joto.
Kwa mujibu wa TMA, viwango vya joto la chini vinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 6°C hadi 21°C katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, huku Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki zikitarajiwa kuwa na joto la kati ya 10°C na 20°C. Kanda ya Kusini inatarajiwa kuwa na viwango vya nyuzi joto 8°C hadi 22°C, wakati maeneo mengine ya nchi yanatarajiwa kuwa kati ya 10°C na 25°C.
Aidha, TMA imewakumbusha wananchi kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019, mamlaka hiyo ndiyo taasisi yenye jukumu na mamlaka ya kutoa taarifa za utabiri na tahadhari za hali ya hewa kwa umma.
TMA imeonya kuwa kutoa au kusambaza taarifa zisizo rasmi kuhusu hali ya hewa ni kosa kisheria kwa mujibu wa vifungu vya 27, 31(5) na 46(1) vya sheria hiyo.
#tma #haliyahewa #aphelion #tanzania #baridi

Hakuna maoni: