KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026 AMPONGEZA MENEJA TARURA MULEBA KWA USIMAMIZI MZURI WA MIRADI

‎Muleba, Kagera.

‎Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu. Wazo Mwang’onda amempongeza Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Muleba Mhandisi Dativa Telesphory kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

‎Mwang’onda ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru wilayani Muleba akieleza kuwa usimamizi madhubuti wa miradi ni msingi muhimu wa kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinatumika ipasavyo na kuleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.

‎Amesema Mhandisi Dativa ambaye pia Mratibu wa Mwenge wa Uhuru wilayani humo ameonesha mfano mzuri wa namna wataalamu wanavyoweza kutumia taaluma zao kuchochea maendeleo ya wananchi.

‎"Napenda kumshukuru na kumpongeza Meneja wa TARURA wilayani Muleba kwa kazi nzuri anayoifanya. Pia ninaomba wahandisi wengine kama alivyo Mhandisi Dativa waisaidie wilaya ya Muleba ili iweze kusonga mbele kwenye maendeleo kwa sababu maendeleo yanakwenda kwenye miradi inayohusisha ujenzi ikiwemo barabara na majengo kwahiyo wahandisi wajitoe kimasomaso kuinua maendeleo nchini", amesema Mwang’onda.

‎Aidha, Mwang’onda amewaomba viongozi wa serikali wilayani Muleba kuendelea kuwa wasimamizi wazuri wa miradi inayotekelezwa katika maeneo yao akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila fedha inayotolewa na serikali inazaa matokeo yanayoonekana na yenye manufaa kwa wananchi.

‎Amesema serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali hivyo ni wajibu wa viongozi na watendaji kuhakikisha rasilimali hizo zinaleta thamani halisi kwa wananchi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.