Dar es Salaam.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ametangaza kuanza rasmi kwa Kampeni ya Kitaifa ya “Septemba ya Utambulisho”, huku akiwataka wananchi wenye vitambulisho vya NIDA vilivyokamilika kwenda kuvichukua ili kukamilisha safari yao ya utambulisho.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msigwa amesema kampeni hiyo inaanza Septemba 1 na itaendelea hadi Septemba 30, 2026, katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) zilizopo wilaya mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Siku ya Utambulisho Duniani inayoadhimishwa Septemba 16.
Amesema hadi Julai 2026, jumla ya watu 27,458,882 walikuwa wamesajiliwa na NIDA, sawa na asilimia 87.2 ya watu milioni 31.47 wenye umri wa miaka 18 na zaidi waliotajwa katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Aidha, vitambulisho milioni 21,526,585 vilikuwa vimezalishwa, huku milioni 20,935,351 vikiwa tayari vimegawiwa kwa wananchi.
Msemaji huyo amesema mfumo wa NIDA umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kurahisisha huduma za kijamii na kiuchumi, ambapo hadi Agosti 2026 jumla ya taasisi 157, zikiwemo 72 za Serikali na 85 za sekta binafsi, zimeunganishwa na mfumo huo kwa ajili ya kuhakiki taarifa za wananchi.
Ameeleza kuwa mfumo huo umesaidia katika maeneo mbalimbali, ikiwemo usalama na udhibiti wa uhalifu, usajili wa walipakodi kupitia TRA, usajili wa laini za simu kupitia TCRA, huduma za kifedha, afya kupitia NHIF, mikopo ya elimu ya juu kupitia HESLB, malipo kwa walengwa wa TASAF pamoja na kurahisisha usajili wa biashara na kampuni kupitia taasisi mbalimbali.
Wakati huo huo, Msemaji Mkuu wa Serikali amewataka wananchi kutokabidhi vitambulisho au namba zao za NIDA kwa watu wengine kwa ajili ya kusajili laini za simu au huduma nyingine, akisema kitendo hicho kinaweza kuwafanya wawajibike endapo taarifa zao zitatumika katika uhalifu. Aidha, amezitaka taasisi za umma na binafsi kujiunga na mfumo wa uhakiki wa NIDA ili kuongeza usalama na uaminifu katika utoaji wa huduma.
Akitangaza kaulimbiu ya Tanzania kwa mwaka 2026, Msemaji Mkuu wa Serikali amesema ni “KIPO, KICHUKUE, KAMILISHA SAFARI YAKO,” huku akiwasihi wananchi ambao vitambulisho vyao vimekamilika na vipo katika ofisi za NIDA kwenda kuvichukua ili kukamilisha safari yao ya utambulisho na kupata fursa ya kunufaika na huduma mbalimbali zinazotumia mfumo wa NIDA.

Hakuna maoni: