MGOGORO WA ARDHI MADALE: FAMILIA YA MUSHI YAFUNGUKA, YAOMBA NDUGU ZAO WALIOKAMATWA KUACHIWA

DAR ES SALAAM

Familia za David Mushi na Mariam Mongi zimepinga sababu zilizotolewa za kukamatwa kwa baadhi ya wanafamilia, zikisema hazikupata taarifa wala wito wa kuhudhuria ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika eneo la Madale, Kinondoni, Septemba 19, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwanasheria wa familia hizo, Wilson Ogunde, familia ilikuwa imeshiriki kikao cha usuluhishi kuhusu mgogoro huo Septemba 18, 2026, kilichoongozwa na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi. Amesema baada ya kikao hicho, baadhi ya wanafamilia waliambiwa wanaweza kurejea Moshi na kwamba watajulishwa iwapo watahitajika tena.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya familia kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu agizo la Mkuu wa Mkoa la kutaka wanafamilia wakamatwe, baadhi yao walirejea Dar es Salaam na kujitokeza kwa hiari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kabla ya kwenda Kituo cha Polisi Oysterbay, ambako waliwekwa chini ya ulinzi.

Familia imesema waliokamatwa ni pamoja na bibi wawili na vijana watatu, huku mmoja wa wanawake hao akiwa na umri wa miaka 86 na akihitaji huduma maalum za kiafya. Mwanasheria Ogunde ameomba mamlaka kuzingatia hali hiyo na kupitia upya hatua ya kuwashikilia wanafamilia hao.

Hatua hiyo inafuatia ziara ya RC Chalamila katika eneo la Madale, ambako alikwenda kushughulikia mgogoro wa ardhi unaohusisha familia ya Mushi na wananchi waliokuwa wamejenga katika eneo hilo. Taarifa ya Manispaa ya Kinondoni inathibitisha kuwa ziara hiyo ilifanyika Septemba 19, 2026, kwa lengo la kushughulikia mgogoro huo na kutafuta suluhisho.

Katika taarifa yake, familia imesema umiliki wake wa eneo hilo umewahi kuthibitishwa katika hatua mbalimbali za mahakama na kwamba utekelezaji wa hukumu ulifanyika Septemba 3, 2026 kupitia dalali wa mahakama chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi. Familia pia imeeleza kuwa imekuwa ikishiriki vikao mbalimbali vya usuluhishi vilivyoitishwa na mamlaka za serikali.

Kwa upande wake, taarifa zilizoripotiwa wakati wa ziara hiyo zilieleza kuwa RC Chalamila alikerwa na kutokuwepo kwa familia ya Mushi katika mkutano aliouitisha na akaagiza wanafamilia watafutwe na kukamatwa. Chalamila alieleza kuwa lengo la serikali halikuwa kutengua uamuzi wa mahakama, bali kuwakutanisha wahusika na kutafuta suluhisho la mgogoro huo kwa amani.

Familia hiyo sasa imeomba mamlaka kupitia upya hatua ya kuwashikilia ndugu zao, huku ikilitaka Jeshi la Polisi kuzingatia haki zao, ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 86. Pia imeomba mamlaka za uchunguzi kuchunguza madai ya uuzaji wa vipande vya eneo hilo wakati shauri likiendelea mahakamani.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.