DAR ES SALAAM.
Mkutano Mkuu wa Mwaka (Jalsa Salana) wa 55 wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya nchini, unaotarajiwa kufanyika Septemba 25 hadi 27, 2026, unalenga kuongeza hofu ya Mwenyezi Mungu na uchamungu (Taqwa) mioyoni mwa washiriki.
Mkutano huo unaotarajiwa kuhudhuriwa na washiriki takribani 5,500 kutoka maeneo mbalimbali, utafanyika katika eneo maarufu la Ahmadiyya lililopo Kitonga, Kata ya Msongola, Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na wanahabari Septemba 22, 2026 jijini Dar es Salaam, Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Khawaja Muzaffar Ahmad, amesema utaratibu wa kufanyika kwa Jalsa Salana ulianzishwa na mwanzilishi wa jumuiya hiyo, Hadhrat Mirza Ghulam Ahmad.
Amesema mwanzilishi huyo alitumwa na Mwenyezi Mungu kutimiza bishara za ujio wa Imam Mahdi pamoja na ujio wa Masihi katika zama hizi, ambazo zilielezwa na Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.) pamoja na waanzilishi wa dini nyingine duniani.
"Mkutano huu unafanyika ili kuongeza hofu ya Mwenyezi Mungu mioyoni mwa washiriki, kupata Taqwa, kumjali Mungu, kuepukana na mabaya, kuwa na moyo wa huruma na kuongeza upendo baina yao," amesema Sheikh Khawaja.
Amebainisha kuwa mkutano huo utahudhuriwa pia na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini na viongozi wa kijamii, ambao watatoa nasaha kwa washiriki.
Amesema hotuba na nasaha mbalimbali zitatolewa na wataalamu wa jumuiya hiyo, zikijikita katika mada mbalimbali, ikiwemo maisha ya Mtume Muhammad (s.a.w.) kama chemchemi ya Taqwa na uchamungu, mafundisho ya Masihi, malezi bora ya familia pamoja na mafanikio katika maisha ya mtu.
Amesisitiza kuwa kaulimbiu ya Jalsa Salana ya mwaka huu ni “Taqwa (Uchamungu) Ndiyo Mzizi wa Kila Wema”, ikiwa na lengo la kuwakumbusha waumini umuhimu wa kuwa na Taqwa kwa kutekeleza maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na makatazo yake, kwa lengo la kupata radhi na mapenzi ya Mungu.
Pia amesema washiriki wenye afya njema na wanaokidhi vigezo vya umri watapata fursa ya kuchangia damu kupitia Benki ya Taifa ya Damu Salama.
Aidha, amesema hotuba zote za Jalsa Salana ya mwaka huu zitasikika mubashara kupitia Redio Ahmadiyya Mtwara pamoja na tovuti ya redio hiyo, radioahmadiyya.or.tz.
Sheikh Khawaja amesema jumuiya hiyo inalenga kueneza ujumbe wa amani kwa Waislamu na jamii duniani kote, huku ikiwa mstari wa mbele kupinga tafsiri na misimamo inayohusishwa na Uislamu, ikiwemo matumizi ya upanga katika jihadi, ugaidi, kutotii serikali zisizo za Kiislamu na misimamo mikali isiyovumilia wengine.

Hakuna maoni: