DAR ES SALAAM:
SERIKALI imetoa Shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuendelea na malipo ya fidia kwa wananchi wa Kipunguni, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kumaliza madeni ya fidia kwa wananchi kwa awamu.
Mkurugenzi wa Fedha na Uhasibu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mohamed Seif, amesema jumla ya wafidiwa 1,864 wamehakikiwa, ambapo wananchi 717 tayari wamelipwa fidia zao.
Amesema wafidiwa 1,147 ndio waliosalia kulipwa, huku TAA ikiwa tayari imepokea Shilingi bilioni 20 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kuendelea na zoezi hilo.
Kwa mujibu wa Seif, hadi sasa jumla ya Shilingi bilioni 86 zimeshapokelewa na kutumika katika malipo ya fidia, kati ya jumla ya Shilingi bilioni 144 zinazotakiwa kulipwa.
Amesema baada ya kupatikana kwa Shilingi bilioni 20 za awamu hii, kiasi kinachobaki kulipwa ni Shilingi bilioni 58.
Seif amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ina dhamira ya kumaliza deni lote la fidia ili kila mwananchi mwenye stahiki alipwe fedha zake kwa wakati.
Amesema wananchi waliopo kwenye orodha ya watakaolipwa katika awamu hii watapewa fomu maalum kupitia Wenyeviti wa Mitaa na Serikali za Mitaa.
Baada ya kujaza fomu hizo, wananchi watawasilisha benki kwa ajili ya uhakiki wa taarifa zao, kisha fomu hizo zitarejeshwa TAA kwa hatua zinazofuata.
Aidha, TAA itawaita wananchi husika kwa ajili ya kufanya uhakiki wa mwisho kabla ya malipo kukamilishwa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Athumani Mbombokaleo, amesema zoezi la malipo linaanza rasmi Jumatatu, Septemba 28, 2026, huku akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kila mwananchi anayestahili anapata haki yake.
“Tunachukua nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Kipunguni na maeneo mengine kwa uvumilivu wao. Zoezi hili ni endelevu na kila mwenye haki atalipwa kulingana na awamu zitakavyopangwa,” amesema Mbombokaleo.
Amesema majina ya wananchi watakaolipwa katika awamu hii yatapelekwa kwa Wenyeviti wa Mitaa na Serikali za Mitaa, ambapo wahusika watapewa fomu maalum za kujaza taarifa za akaunti zao za benki.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo, uhakiki wa taarifa za akaunti za benki utafanyika wiki hii kabla ya malipo kuanza rasmi Jumatatu.
Aidha, Serikali imewataka wananchi ambao majina yao hayataonekana katika awamu hii kuwa wavumilivu, kwa kuwa malipo yataendelea kufanyika kwa awamu kadri fedha zitakavyopatikana.

Hakuna maoni: