Dar es Salaam.
Fursa za kuongeza ajira, kukuza uwekezaji na kutumia rasilimali za bahari na maji kwa njia endelevu zinatarajiwa kutawala mjadala katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu, ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Septemba 7 hadi 9, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha wataalamu, watafiti, watunga sera na wadau mbalimbali kutoka Tanzania, Afrika na mataifa mengine duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Dk. Tumaini Gurumo, alisema kongamano hilo litajadili namna ya kutumia rasilimali za bahari, mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji kwa njia endelevu ili kuongeza manufaa kwa wananchi na taifa.
Gurumo alisema pia kutakuwa na mawasilisho ya kitaalamu na tafiti mbalimbali zinazohusiana na Uchumi wa Buluu, kwa lengo la kubaini changamoto zinazoikabili sekta hiyo, kutafuta suluhisho na kuweka mikakati ya kutumia matokeo ya tafiti katika kukuza uchumi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Aidha, alisema vijana kutoka vyuo vikuu, shule za sekondari na shule za msingi wamealikwa kushiriki kongamano hilo ili kupata uelewa kuhusu fursa zinazopatikana kupitia Uchumi wa Buluu, hususan katika ajira, ujasiriamali, uwekezaji, teknolojia, utafiti na ubunifu.
Kongamano hilo linatarajiwa kushirikisha washiriki kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Ghana, Afrika Kusini, Comoro, Seychelles, Uganda, Japan, Sweden na Urusi, pamoja na mabalozi, viongozi wa serikali na taasisi binafsi, wanasayansi, watafiti, watunga sera na wadau wengine wa sekta hiyo.
Gurumo alisema kongamano hilo linaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, akisisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali za maji kwa njia endelevu ili kuongeza mchango wa Uchumi wa Buluu katika maendeleo ya taifa.


Hakuna maoni: