DAR ES SALAAM.
Wananchi wamepewa nafasi ya kuamua kazi za uandishi wa habari na makala za maendeleo wanazoona zimeleta mchango mkubwa kwa jamii na kuchochea maendeleo ya Taifa, kupitia zoezi la upigaji kura la Tuzo za Samia Kalamu Awards 2026.
Zoezi hilo limeanza leo Septemba 3, 2026 na linatarajiwa kukamilika Septemba 30, huku Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Peter P. Mwasalyanda, akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo.
Mwasalyanda amesema kura za wananchi ni sehemu muhimu ya mchakato wa kumpata mshindi, kwani zinatoa fursa kwa watumiaji wa habari kutambua na kuunga mkono kazi zilizoakisi mahitaji ya jamii, kuibua masuala muhimu ya maendeleo na kuleta athari chanya katika maisha ya watu.
Amesema jumla ya kazi 3,003 zilizowasilishwa na waombaji 985 zilifanyiwa tathmini na jopo la majaji, ambapo kazi 294 zilizopata alama za juu zimefuzu kuingia hatua ya kupigiwa kura na wananchi.
Wananchi wanaweza kushiriki kupiga kura kupitia tovuti rasmi ya tuzo www.samiaawards.tz, au kutuma ujumbe mfupi wenye neno “SKA” likifuatiwa na namba ya mshiriki kwenda 15200.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Samia Kalamu Awards, Dkt. Rose Reuben, amesema wananchi ni walaji wa habari, hivyo ushiriki wao ni muhimu katika kutambua kazi bora na maudhui yenye uwezo wa kuitangaza Tanzania kimataifa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Prudence Constantine, amewataka waandishi waliofuzu kuhakikisha kazi zao zinatumika kikamilifu katika kuimarisha maadili, weledi na utafiti katika tasnia ya habari.
Samia Kalamu Awards ni tuzo za kitaifa zilizoanzishwa kwa lengo la kutambua, kuenzi na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari na utayarishaji wa makala za maendeleo nchini Tanzania. Tuzo hizo zinaratibiwa kwa ushirikiano wa TCRA, TAMWA na JAB.







Hakuna maoni: