TALGWU KUFANYA MKUTANO MKUU WA TAIFA SEPTEMBA 17 NA 18

 


DODOMA.

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa Taifa Septemba 17 na 18, 2026, kwa mujibu wa Ibara ya 55.1 ya Katiba ya chama hiyo ya toleo la mwaka 2026.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mratibu wa Uchaguzi wa TALGWU 2026, Shani Kibwasali, amesema mkutano huo utafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper jijini Dodoma.

Amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, huku akieleza kuwa mkutano huo utafuatiwa na Baraza Kuu la Taifa litakalofanyika Septemba 19, 2026.

Amesema miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na kupitia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za chama kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2026.

Aidha, amesema mkutano huo utafanya uchaguzi wa viongozi watakaokiongoza chama kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2031, ambapo kwa sasa Mwenyekiti wa TALGWU ni Tumaini Nyamhokya.

Katika hatua nyingine, Kibwasali ametoa hamasa kwa wanachama wote kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho. 

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.