TUUNGANE KUPIGANIA KATIBA MPYA NA KUKABILIANA NA MKWAMO WA KISIASA NCHINI- DOROTHY SEMU



DAR ES SALAAM.

Chama cha ACT Wazalendo kimewataka Watanzania kuungana na kudai kuanzishwa mara moja kwa mchakato wa Katiba Mpya, kikisema mkwamo wa kisiasa nchini hauwezi kutatuliwa kwa marekebisho madogo au maboresho ya Katiba iliyopo.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 15, 2026, na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Manka J. Semu, katika ujumbe wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, ambapo amesema Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa zinazohusisha uhuru wa habari na kujieleza, hali ya vyama vya upinzani na masuala ya haki za wananchi.

Semu amesema hali hiyo imeendelea kudhihirishwa pia na kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa wakosoaji wa Serikali, pamoja na madai ya kutekwa, kupotea na kuuawa kwa wananchi, huku akitaka kuwepo kwa uwajibikaji wa kutosha katika matukio hayo.

Amesema uchaguzi nchini umeendelea kuonekana kama chanzo cha mateso na migogoro, akidai kuwa vyama vya upinzani vimekuwa vikikabiliwa na mazingira yanayowanyima wananchi fursa ya kutumia kikamilifu haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Kwa mujibu wa Semu, tangu mwaka 2024 hadi sasa, zaidi ya watu 2,046 wamekamatwa kwa tuhuma za uhaini na takribani kesi 1,651 zimefikishwa mahakamani, huku watu wengine 134 wakikamatwa na kufunguliwa kesi zinazohusiana na ugaidi.

Amesema ACT Wazalendo haitaki kuona taifa likirejea katika mazingira ambayo uchaguzi unageuka kuwa chanzo cha maumivu na mateso kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa kulindwa kwa uhuru wa kutoa maoni na vyombo vya habari kufanya kazi bila shinikizo.

Semu amesema Tanzania inahitaji Katiba Mpya itakayoweka misingi imara ya demokrasia, kulinda haki na uhuru wa wananchi, kuweka mipaka ya mamlaka ya dola, kujenga taasisi huru na zinazowajibika na kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.

Ametoa wito kwa wadau wote, wakiwemo wapenda amani na demokrasia, kuungana katika kudai ratiba kamili ya mchakato wa Katiba Mpya, akisema Tanzania inaweza kuwa na Katiba hiyo kabla ya mwaka 2029.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.