DAR ES SALAAM,
Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wameandaa huduma maalum za uchunguzi wa afya ya moyo kwa abiria wanaosafiri na treni ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Huduma hizo zitatolewa bure kuanzia Septemba 21 hadi 27, ambapo wataalamu na mabingwa wa afya ya moyo kutoka JKCI watasafiri ndani ya treni hiyo na kuwafanyia abiria vipimo mbalimbali, ikiwemo Echo, ECG, sukari na mafuta kwenye damu.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema mpango huo umeandaliwa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yanayofanyika Septemba 29 kila mwaka.
Amesema vipimo hivyo ambavyo vikitolewa hospitalini vinaweza kugharimu zaidi ya Sh500,000, lakini katika wiki hiyo abiria watapata huduma hizo bila malipo wakiwa safarini.
Amesema TRC ipo katika hatua za usanifu wa mabehewa maalum yatakayokuwa na vifaa vya matibabu na vitanda kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa mahututi na wanaopewa rufaa kutoka mikoani kwenda hospitali kuu, huku mpango huo ukitarajiwa kuanza ndani ya miezi sita ijayo.
Viongozi hao wamewataka abiria na wananchi kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.


Hakuna maoni: