Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Serikali imesema awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango wa bima ya afya itafungua fursa kwa Watanzania wote kujiunga, huku ikiendelea kukamilisha usajili wa kaya maskini.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba kutoka Wizara ya aAfya,Emmanuel Tayari, wakati wa uzinduzi wa kituo kilichoboreshwa cha matibabu ya kinywa na meno pamoja na huduma za vipandikizi katika Hospitali ya Aga Khan.
Tayari amesema katika awamu hiyo, pamoja na kukamilisha usajili wa kaya maskini, dirisha litafunguliwa kwa makundi yote maalum na hatimaye wananchi wote wataruhusiwa au kuhamasishwa kujiunga na mfumo huo.
Amesema utaratibu kamili wa namna wananchi watakavyoweza kujiunga na awamu hiyo utatangazwa hivi karibuni.
«“Katika awamu ya pili tutamalizia kusajili zile kaya maskini, lakini tutafungua kwa makundi yote maalum. Kwa maana hiyo, Watanzania wote watakaribishwa au kuhamasishwa kujiunga,” amesema.»
Katika hatua nyingine, Tayari amesema suala la malipo kwa hospitali binafsi halijawa kikwazo katika mfumo wa bima ya afya, akieleza kuwa hospitali hizo zimeendelea kuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mfumo huo.
Kwa mujibu wa takwimu alizotoa, takribani asilimia 60 ya malipo ya bima ya afya yanaelekezwa kwenye hospitali binafsi, jambo linaloonyesha nafasi ya sekta hiyo katika utoaji wa huduma za afya kwa wanachama wa bima.
Amesema ushirikiano kati ya mifumo ya bima ya afya na hospitali binafsi unaendelea kuimarika, akitolea mfano Hospitali ya Aga Khan ambayo hivi karibuni ilisaini mkataba na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuendelea kutoa huduma kwa wanachama wa mfuko huo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Profesa Muzdalifat Abeid, amesema uwekezaji katika kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa hospitali hiyo wa kuongeza huduma maalumu zenye viwango vya juu, kwa lengo la kupunguza idadi ya Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.
Amesema huduma hizo sasa zinapatikana pia kwa wanachama wa NHIF baada ya hospitali hiyo kusaini mkataba na mfuko huo.
«“Tumefanya uzinduzi wa dental clinic, ambao ni sehemu ya upanuzi mkubwa wa huduma zetu. Tunaendelea kuwekeza katika huduma za viwango vya juu ili kupunguza safari za watu kwenda nje ya nchi kutafuta huduma hizi,” amesema.
Profesa Abeid amesema uzinduzi huo haumaanishi kuanzishwa kwa idara mpya, bali ni upanuzi na ujumuishaji wa huduma za meno katika mfumo wa huduma za hospitali na jamii.
Amesema hospitali hiyo imekuwa ikiendesha programu mbalimbali za kutoa elimu kuhusu afya ya kinywa na meno, pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya meno na kampeni katika shule, taasisi na jamii.
Kwa mujibu wa Profesa Abeid, hatua hiyo inalenga kusogeza huduma maalumu karibu na wananchi, huku wagonjwa wakipata huduma kwa wakati na kwa viwango vya juu.
Aidha, Profesa Abeid amesema huduma hizo zinaifanya Hospitali ya Aga Khan kuwa miongoni mwa hospitali binafsi zinazotoa huduma maalumu za meno nchini, huku akieleza kuwa uwekezaji huo hautakuwa wa mwisho.
Amesema hospitali hiyo itaendelea kuwekeza katika huduma nyingine maalumu ili kuongeza wigo wa matibabu yanayopatikana nchini.
«“Safari yetu haijaishia hapo. Tutaendelea kuwekeza na kufungua huduma nyingine maalumu ili kuongeza wigo wa huduma zinazopatikana nchini,” amesema.»



Hakuna maoni: