TISEZA YAWAFICHULIA WAWEKEZAJI FURSA KANDA YA ZIWA


Na Mwandishi wetu

Geita

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imewafichulia wawekezaji fursa mbalimbali zilizopo Kanda ya Ziwa, zikiwemo madini, viwanda vya uchenjuaji, uchakataji wa mazao ya uvuvi pamoja na uzalishaji wa bidhaa na huduma zinazohudumia sekta ya madini.

Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Mjumbe wa Bodi ya TISEZA, Absolom Kibanda, amesema ushiriki wa mamlaka hiyo unalenga kutoa elimu ya uwekezaji, kuitambulisha TISEZA kwa wananchi na wawekezaji, pamoja na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali kwa urahisi kupitia mfumo wa One-Stop Centre.

Kwa upande wake, Meneja wa TISEZA Kanda ya Ziwa, Venance Mashiba, amesema mamlaka hiyo imeshirikiana na zaidi ya taasisi 16 katika maonyesho hayo, ikiwemo TMDA, BRELA, TBS na TRA, ili kuwawezesha wawekezaji kupata maelekezo na huduma zinazohitajika katika kuanzisha na kuendesha biashara, ikiwemo usajili, vibali na masuala ya kodi.

TISEZA imetaja mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu kuwa na fursa mbalimbali za uwekezaji katika madini, uvuvi, kilimo na viwanda.

Geita imetajwa kuwa na fursa kubwa katika uchenjuaji na shughuli nyingine za mnyororo wa thamani wa madini, huku eneo la Buzwagi Kahama likitajwa kuwa na fursa za viwanda vya bidhaa na huduma kwa migodi.

Aidha, Bunda mkoani Mara limetajwa kuwa na fursa katika viwanda mchanganyiko, ikiwemo uchakataji wa mazao ya uvuvi, ufugaji wa samaki na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na samaki. 

TISEZA imewataka wawekezaji kutumia fursa hizo kuongeza thamani ya rasilimali, uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.