MZIZIMA FESTIVAL KUAMSHA TAMADUNI ZA KALE, KUUNGANISHA VIZAZI

Dar es salaam.

Watanzania wa rika na makabila mbalimbali wanatarajiwa kukutana katika Tamasha la Mzizima Festival litakalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 11 hadi 13, 2026, kwa lengo la kufufua mila, desturi na tamaduni za kale pamoja na kurithisha urithi huo kwa vizazi vijavyo.

Tamasha hilo lililoandaliwa na Batuta Organization litajumuisha shughuli mbalimbali za kitamaduni, michezo ya jadi, burudani na mijadala ya historia na maadili. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Pamoja Tutashinda Tanzania (PATUTA), Dkt. Aidan Ndaombwa, amesema vikundi 26 vya ngoma za asili kutoka makabila mbalimbali nchini vinatarajiwa kushiriki, huku mazungumzo na vikundi hivyo yakiendelea.

Amesema vijana watapata fursa ya kujifunza michezo ya jadi ikiwemo bao, pamoja na kufahamu historia ya usafiri wa umma jijini Dar es Salaam, kuanzia chimbuko la daladala na UDA hadi maendeleo ya usafiri wa mwendokasi. Historia ya jiji hilo kama kitovu cha biashara pia itajadiliwa, ikiwemo maendeleo ya Soko la Kariakoo na mchango wa wafanyabiashara kutoka maeneo na makabila mbalimbali.

Dkt. Ndaombwa ameongeza kuwa kutakuwa na mijadala itakayowakutanisha vijana na wazee waliowahi kushiriki katika masuala ya siasa, utamaduni na majeshi ili kueleza historia na mabadiliko ya jamii. Amesema hatua hiyo inalenga pia kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa maadili kwa kurejesha mshikamano uliokuwa ukijengwa kupitia michezo na shughuli za kitamaduni.

Kwa upnde wake, Mratibu wa tamasha hilo, Mayasa Jabiri, amesema jina Mzizima linaakisi historia ya Dar es Salaam na utamaduni wa ukarimu, huku tamasha hilo likilenga kuitangaza Tanzania kama nchi yenye amani, fursa za kiuchumi na utamaduni unaowakaribisha wageni. Ameeleza kuwa waandaaji wanashirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuhakikisha tamasha linaonyesha utamaduni halisi wa Tanzania.

Naye Afisa Sanaa wa BASATA, Gabriel Awe, amesema baraza hilo limeunga mkono maandalizi ya tamasha hilo baada ya waandaaji kupata mwongozo kuhusu taratibu za kuandaa matamasha nchini. Amewahimiza wadau na wadhamini kujitokeza kuunga mkono tamasha hilo, akieleza kuwa ni jukwaa la kuenzi utamaduni na kujenga uelewa wa maadili kwa kizazi kipya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa VOT AFRIKA LIMITED, Everest Oende, amezitaka kampuni na taasisi mbalimbali kutumia tamasha hilo kuonyesha mchango wao katika shughuli za kijamii na kuhifadhi urithi wa taifa. Waandaaji pia wameandaa mavazi ya kukumbusha mitindo ya zamani, yakiwemo mashati ya Bahama, huku shughuli za tamasha zikitarajiwa kuanza asubuhi hadi usiku kwa siku zote tatu. Watanzania, familia na wadau wamealikwa kujitokeza kushiriki.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.