DC TANGANYIKA AWASISITIZA MAAFISA NA ASKARI WA TAWA KUISHI VIAPO VYAO

Na Beatus Maganja, 

Katavi

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu amewataka Maafisa na Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuishi viapo vyao kwa kutekeleza kwa ujasiri na uadilifu jukumu la kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha urithi huo unafika salama kwa vizazi vijavyo.


Mhe. Buswelu ametoa wito huo Oktoba 4, 2026 wakati akihitimisha mafunzo ya mabadiliko ya mfumo wa utendaji kazi kutoka kiraia kwenda kijeshi kwa Maafisa na Askari 83 wa TAWA katika Kituo cha Mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi, Mlele mkoani Katavi. “Muwe hodari, msiwe wanyonge wala msikatishwe tamaa. Ilindeni nchi yenu na rasilimali zake ili kuhakikisha urithi huu unafika salama kwa vizazi vijavyo,” amesema.


Aidha, ameiomba Menejimenti ya TAWA kuweka mikakati madhubuti ya ulinzi wa rasilimali hizo kwa kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali hususan wananchi wanaoishi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa, huku akiwataka wananchi kuheshimu sheria zinazosimamia maliasili.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi ambaye pia ni Kamanda wa Kanda ya Magharibi Wilbright Munuo, amesema Mamlaka inaamini kuwa maarifa waliyoyapata wahitimu hao yatasaidia kuimarisha utendaji wao, hivyo akawataka kutekeleza majukumu kwa weledi, nidhamu na ukakamavu.

Munuo amesema maeneo ya wanyamapori na misitu yanakabiliwa na shinikizo la shughuli za kibinadamu, zikiwemo ukataji miti hovyo, kilimo na mifugo, ambazo zinachangia uharibifu wa makazi ya wanyamapori, hivyo kuhitaji juhudi zaidi katika kuyasimamia na kuyalinda.

Pia amewataka kuongeza juhudi katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ili kupunguza madhara kwa wananchi na mali zao, sambamba na kuhakikisha uwiano kati ya usalama wa jamii na uendelevu wa rasilimali za wanyamapori unakuwa sawia.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi Wizara ya Maliasili na Utalii, Afisa Mhifadhi Mkuu Patrick Kutondolana amewasisitiza wahitimu hao kutumia maarifa na stadi walizopata pamoja na kuzingatia kiapo walichoapa, akisema kufanya hivyo kutasaidia kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo nchini

Katika mafunzo hayo, Maafisa na Askari hao wamejengewa uwezo katika doria na ujanja wa porini, matumizi ya nguvu ya kadiri, Amri za Jumla za Jeshi la Uhifadhi, huduma ya kwanza, uzalendo, itifaki na maadili, utimamu wa mwili, nidhamu ya kijeshi, matumizi ya ramani na GPS pamoja na sheria za uhifadhi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.